Waziri awaita Takukuru hofu ulaji mradi wa maji

20Jul 2019
Renatha Msungu
KONDOA
Nipashe
Waziri awaita Takukuru hofu ulaji mradi wa maji

SERIKALI imesema itashirikiana na Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi kujiridhisha na utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Masange wilayani Kondoa.

TAKUKURU.

Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso, aliyasema hayo alipozungumza na wananchi wa kijiji hicho katika ziara yake ya kukagua miradi ya maji ukiwamo huo uliogharimu Sh. milioni 433.288.

Alisema atawashirikisha Takukuru kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa mradi huo kutokana na kutoridhishwa na maelezo yaliyotolewa kwake na mkandarasi wa mradi huo.

Mradi huo umetekelezwa chini ya usimamizi wa Kampuni ya Best One.

“Haiwezekani tukauziwa mbuzi kwenye gunia, lazima tukague na kujionea wenyewe baada ya kupewa majibu ya kusuasua. Tutashirikiana na Takukuru ili kubaini ubadhirifu na mkandarasi asilipwe mpaka tujiridhishe na uchunguzi," Aweso alisema.

Awali, akitolea ufafanuzi kuhusu hoja mbalimbali zilizowasilishwa kwake na wananchi wa kijiji hicho kuhusu sekta ya maji, Aweso aliwataka wananchi kuwa na subira, akiwaahidi kuchimbwa visima viwili kijijini huko hivi karibuni.

Alisema taratibu za upatikanaji wa gari la kuchimba visima hivyo zinashughulikiwa.

Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, Dk. Ashatu Kijaji (CCM), alisema yuko tayari kufanya kazi usiku na mchana kutekeleza alichoagizwa na wananchi wa jimbo hilo.

Dk. Ashatu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, alisema adha kubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Masange ni ugumu wa upatikanaji wa maji, hivyo kuna haja Serikali kuchukua hatua za haraka kutatua kero hiyo.

Akisoma taarifa ya mradi wa maji wa kijiji hicho mbele ya Aweso, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Kondoa, Falaura  Kikusa, alisema mradi huo ulianza Desemba 15, 2014 na ulizinduliwa rasmi Septemba 13, 2016 kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru ukigharimu Sh. milioni 433.

Alibainisha kuwa muda wa utekelezaji wa mradi huo kwa mujibu wa mkataba ni miezi minne kuanzia tarehe waliokabidhiwa ambayo ni Desemba 15, 2014 hadi Machi 15, 2015.

Alisema kutokana na changamoto mbalimbali, hususani  kuchelewa kwa malipo ya madai ya mkandarasi, mradi uliongezwa muda wa utekelezaji na kutakiwa kukamilika rasmi Juni 7, 2018.

Alisema kijiji hicho kinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kutokana na ongezeka la wakazi na kukua kwake.

Alibainisha kuwa uwezo wa chanzo cha maji kilichopo ni kutoa lita 119,577.6 kwa siku wakati mahitaji halisi kwa sasa ni zaidi ya lita 141,560 kwa siku.

Kaimu meneja huyo pia alibainisha kuwa mkandarasi wa mradi huo hadi sasa ameshalipwa Sh. milioni 347.421 kati ya Sh. milioni 433.288.