Waziri aweka msimamo matumizi fedha za kigeni 

16Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waziri aweka msimamo matumizi fedha za kigeni 

Serikali imesema haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini, bali imechukua hatua ya kudhibiti matumizi yake ili kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema hayo jana  alipokutana na wawakilishi wa wafanyabiashara mkoani Arusha kujadiliana mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya  biashara nchini. 

Alisema sheria haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini, lakini inasisitiza kuwa watu wanapaswa kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya nchi.

“Tatizo kubwa tunalokumbana nalo ni uhuru ulioachiwa ambao unasababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu kwani kila mmoja anaweza kutumia fedha za kigeni, pia watumiaji wa fedha za kigeni hawafuati thamani ya fedha iliyoko sokoni kila mmoja anakuwa na kiwango tofauti cha thamani ya kubadili fedha za kigeni,” alifafanua Dk. Kijaji.

Ili kuondoa changamoto hizo, alisema serikali imeamua kurekebisha sheria ya matumizi ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu inayozitaka  bei zote nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania. Bei hizo zinajumuisha kodi za nyumba za kuishi na ofisi, bei za ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki. 

“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja ambao si wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Hata hivyo, mlengwa akitaka kulipa kwa Shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa kwa fedha za kigeni,” alisema. 

Aidha, alisema viwango vya kubadilishia fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu zingine, vimetakiwa kuwekwa wazi na visizidi vile vya sokoni. 

Alisema mkazi yeyote wa Tanzania au mtu wa nje anayeishi Tanzania  asilazimishwe kufanya malipo yoyote kwa kutumia fedha za kigeni kama ana Shilingi ya Tanzania mkononi mfano gharama za shule na hoteli.

Aidha Serikali imeagiza vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaokiuka maagizo hayo yaliyotolewa na Serikali.

Naibu Waziri Dk. Kijaji alitoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuhimiza matumizi ya sarafu ili kukuza thamani ya Shilingi, hivyo kusaidia kuinua uchumi wa nchi. 

Habari Kubwa