Waziri: Boresheni Sekta Kilimo JKU

30Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Waziri: Boresheni Sekta Kilimo JKU

​​​​​​​WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum ya SMZ, ameutaka uongozi wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Zanzibar kuwa wabunifu zaidi katika Sekta ya Kilimo na kuhakikisha wanatimiza malengo ya kujitosheleza kwa chakula kwa jeshi hilo kwa kutumia ardhi ya kilimo waliyonayo.

Masoud Ali Mohamed.

Masoud Ali Mohamed aliagiza hayo jana alipozuru kwenye kambi za jeshi hilo huko Bambi, Wilaya ya Kati Unguja.

Alisema majukumu ya JKU ni kubuni mipango itakayoliwezesha jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula kwa kutumia ardhi kwa shughuli za kilimo katika kambi walizonazo.

Alisema bado uongozi wa jeshi hilo haujatumia vizuri ardhi kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali ambayo yatawawezesha kujitosheleza kwa chakula na kujitegemea.

"Nimetembelea shughuli za kilimo katika kambi za JKU, lakini sijaridhishwa na shughuli za kilimo kikiwamo cha mpunga ambacho kama mtakitumia vizuri, mnaweza kujitosheleza kwa chakula," alisema.

Mkuu wa Kambi ya JKU, Luteni Suleiman Benjamin Simon, alisema kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Misri wamefanikiwa kulima mboga nyingi pamoja na matikiti na wameingiza mapato kwa jeshi hilo.

Alisema kwa sasa wamejikita katika kilimo cha viungo ikiwamo vanila na pilipili manga ambazo bei yake ni nzuri katika soko la dunia.

"Tumeanza kulima mazao ya viungo ikiwamo vanila kwa kutumia njia za kitaalamu pamoja na pilipili manga ambapo bei yake katika soko la dunia ni nzuri na yenye tija," alisema.

JKU ilianzishwa kama kambi za vijana baada ya mapinduzi na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume na miongoni mwa majukumu yake ni kulima kwa kutumia mabonde ya kilimo yaliyopo katika kambi zake.