Waziri Mpango atajwa kikwazo kwa viwanda

19May 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Waziri Mpango atajwa kikwazo kwa viwanda

WABUNGE wamebainisha changamoto zinazokwamisha maendeleo ya viwanda nchini huku baadhi yao wakidai Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo kikwazo kikubwa.

Waziri ya Fedha Dk. Philip Mpango.

Waliyasema hayo bungeni mjini hapa jana walipokuwa wanachangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka ujao wa fedha.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alidai Wizara ya Fedha na Mipango inayoongozwa na Dk. Philip Mpango, imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa sekta ya biashara na viwanda kutokana na utaratibu usiofaa wa kuweka vikwazo na kutunga sheria zisizo rafiki kwa sekta husika.

Alisema dhamira ya serikali ya awamu ya tano kujenga uchumi wa viwanda ambao utalijenga taifa kujitegemea inakabiliwa na changamoto ya kutowiana kwa mikakati ya serikali na lengo hilo.

”Mwaka 1967, Mwalimu (Julius) Nyerere aliasisi dhana ya viwanda ambavyo baadaye vilianza kufa. Mwaka jana, nilimuahidi kaka yangu (Charles) Mwijage (Waziri wa Viwanda) na nilionyesha shaka yangu juu ya utekelezaji wa dhamira ya yeye kufikia yale ambayo alikuwa ametarajia na leo tunayaona,” alisema.

Akinukuu taarifa za Benki Kuu (BoT) za mwezi uliopita, Bashe alisema uzalishaji kwenye viwanda nchini umeshuka kutoka Dola za Marekani milioni 1.4 hadi Dola 870,000, maana yake tumepoteza Dola 500, mauzo ya bidhaa zetu nje yameshuka kwa Dola milioni 80, uvuvi na mazao ya samaki yameshuka kwa Dola milioni 20.

Pia alisema mikopo katika sekta ya kilimo  imeshuka kwa asilimia 92, usafirishaji na mawasiliano asilimia 21.6, ujenzi asilimia tatu, hoteli na migahawa asilimia saba.

Kwa upande wa usafirishaji wa mazao ya ndani, Bashe alisema bidhaa pekee iliyokua ni korosho kutokana na kuongezeka kwa bei.

Alisema tumbaku imeshuka kutoka Dola milioni 343 mwaka 2015 hadi Dola milioni 281 Machi 2017, pamba imeshuka kwa dola milioni 10, kahawa Dola milioni tisa, karafuu Dola milioni 13, katani Dola milioni moja.

”Tatizo ni nini? Tatizo ni sera za kodi kutobadilika," alisema. "Mfano Sheria ya Uwekezaji kifungu namba 19, sheria hii tumeibadilisha mwaka 2009 kwa kufuta utaratibu wa 'incapital goods' ikashuka 'investiment' (uwekezaji).

”Tukaibadilisha mwaka 2010, 2012, 2014 na 2015. Tunafuta na kuruidisha wakati ni nchi moja.”

Bashe pia alinukuu ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu kilimo cha biashara, akieleza kuwa ili kuanzisha kiwanda kidogo cha kuzalisha maziwa nchini, unahitaji leseni kutoka Brela, cheti, uthibitisho wa afya ya wafanyakazi na kibali cha kuingiza na kutoa nchini.

Alisema ili kuvipata vitu hivyo, unatakiwa kupitia Brela, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango (TBS), Osha, wizara inayohusika na kazi pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mazingira (NEMC).

“Nani anakuja kuwekeza hapa?” Alihoji Bashe na kuishauri serikali kuzingatia mambo matatu ambayo hivi karibuni Naibu Mkurugenzi wa IFM alisema yanapaswa kuzingatiwa na Tanzania ili kuinua uchumi wake.

Mambo hayo ni kuongeza ajira katika sekta za viwanda na kilimo, 'export duty' na kuongeza gharama za ukuaji wa viwanda.

"Wakati sisi tumeweka 'export duty', ukiingiza kemikali kwa ajili ya ngozi, unailipia kodi asilimia 25 na asilimia 18 ya VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani). Tutawezaje kushindana?" Alihoji.

Dk. Raphael Chegeni (Busega-CCM), aliyeshauri kuwe na ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili kutimiza dhamira ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga (Chadema), aliitaka wizara hiyo kukipa kipaumbele Kiwanda cha Nyuzi Tabora ambacho kimefungwa kwa muda mrefu.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), alisema anaishangaa serikali kwa kutokutenga fedha kupitia Wizara ya Viwanda kwa ajili ya Bandari ya Bagamoyo.

Mbunge wa Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa (CCM), aliiomba serikali kupitia upya fidia walizopewa wananchi wa Bagamoyo kwa maeneo yao yaliyochukuliwa viwanda akidai wengi wao wamepunjwa.

Vedastus Manyinyi, Musoma Mjini (CCM), alisema ili Tanzania ifanikiwe kiuchumi, ni lazima iwekeze katika viwanda vidogo vidogo (SIDO) kwa kuwa huko ndiko kutakakozalisha wataalamu wa kati.

Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM), aliishauri serikali kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji akiamini kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.

Dk. Christina Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), alisema ili viwanda vifanikiwe nchini, ni lazima serikali ihakikishe kuna umeme na maji ya uhakika, kauli ambayo pia iliungwa mkono na wabunge wengi akiwamo Lorensia Bukwimba, Mbunge wa Busanda (CCM).