WB yasaidia miradi ya maji kwa mil. 800/-

27Jun 2017
Said Hamdani
RUANGWA
Nipashe
WB yasaidia miradi ya maji kwa mil. 800/-

BENKI ya Dunia imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, Sh. 846,757,550 zitakazotumika kukamilisha ujenzi wa mtandao wa huduma ya maji.

Miradi hiyo katika vijiji vya Naunambe na Mbekenyera, itakayowafanya wananchi kuondokana na tatizo la kutumia maji yasiyo salama.

Hayo yalielezwa na Mhandisi wa maji wilayani humo, Laurece Mapunda, alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Ruangwa mwishoni mwa wiki.

Mapunda alifafanua kwamba fedha hizo zitatumika kukamilisha miradi ya maji iliyokuwa imekwama miaka minne iliyopita kutokana na kukosekana kwa fedha za kumalizia.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo ulianza 2013/2014, lakini ilisimama kutokana na sababu hizo na kwamba ambapo Benki ya Dunia imeweza kuiipatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Mapunda alisema baada ya kupatikana kwa fedha hizo, utekelezaji wa miradi hiyo katika vijiji hivyo vya Naunambe, Mbekenyera na Mibure umeanza na inatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu kufuatia mkandarasi (bila ya kumtaja jina) kuendelea na kazi.

“Iwapo hakutakuwa na changamoto yoyote, miradi hiyo inatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni na ule wa Mibule Oktoba mwaka huu pia,” alisema Mapunda.

Aidha, alibainisha hivi sasa kazi inaendelea vizuri na tayari takribani asilimia 99.0 imekamilika na kinachosubiriwa ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) waunganishe umeme kwenye  jengo ambalo mtambo wa kusukumia maji umefungwa kupeleka kwa wananchi wa vijiji husika.

“Naweza kusema kazi hii imeshakamilika kwa kiasi kikubwa, tunasubiria Tanesco watuunganishie umeme ili maji yaanze kutumiwa na wananchi,”aliongeza.

Aidha, alisema ujenzi wa mradi uliopo kijiji cha Mibure, unaotarajia kugharimu Sh. 245,496,905, unaendelea vizuri sambamba na ujenzi wa mabomba, vituo 12, tenki la kuhifadhia lenye ujazo wa lita 50,000, unatarajia kukamilika Oktoba mwaka huu.

Alizitaja kazi zingine ambazo fedha hizo zitatumika ni ununuzi na ufungaji wa jenereta ya umeme kwa ajili ya kusukuma maji na kusambaza kwenye vituo vitakavyotumika.

Kwa mujibu wa Mapunda, kukamilika kwa miradi hiyo miwili, zaidi ya wananchi 10,000 wa vijiji hivyo watapata huduma ya majisafi na salama, hivyo kuondokana na changamoto ya kutumia maji yasiyo salama.

Habari Kubwa