Wenye daladala Dodoma wapongeza kuhamishiwa kituo

08Nov 2016
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Wenye daladala Dodoma wapongeza kuhamishiwa kituo

MADEREVA wa mabasi yanayofanya safari nje ya mji wa Dodoma, wamepongeza kuondolewa mjini na kupelekwa kituo kipya cha Kikuyu.

Awali kabla ya kituo hicho hakijahamishwa, walikuwa wakitumia cha Majengo ambacho walidai hakina usalama kwa ajili ya mali zao na abiria.

Akizungumza na Nipashe jana, dereva Haji Ayoub, kwa niaba ya wenzake, alisema wanaipongeza Manispaa ya Halmashauri ya Dodoma kwa kuwaondoka mjini na kuwahamishia Kikuyu ambako kuna nafasi na usalama zaidi.

Ayoub alisema madereva wa mabasi hayo, wanaamini kuhamishwa kwao kutoka katikati ya mji ni lengo la serikali kuuweka mji katika hali ya mpangilio kutokana na hivi sasa serikali kuhamishia makao makuu mjini humo.

Aidha, alisema kwa sasa wanaiomba manispaa kuwajengea vibanda kwa ajili ya mamalishe ili abiria wasipate usumbufu kupata vyakula wanaposafiri kwenda vijijini.

"Tunaomba manispaa isimamie zoezi hili kwa sababu hali ya vyakula katika kituo hiki ni shida kupatikana," alisema Ayoub.

Hata hivyo, Ayoub alisema wao kama madereva wanatarajia kuanzisha chama cha kutatua matatizo yao kama ilivyokuwa awali.

Alisema wanahitaji kuona kituo hicho cha mabasi kinakamilika mapema kwa kuwapo na mahitaji yote muhimu ili abiria wasiweze kupata shida.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia changamoto zilizopo katika kituo hicho, hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi.
Kituo hicho cha mabasi kimeanza kutumika rasmi leo.

Habari Kubwa