Wenye taaluma ujenzi vyoo bora waitwa

18Feb 2019
Nebart Msokwa
Chunya
Nipashe
Wenye taaluma ujenzi vyoo bora waitwa

SERIKALI wilayani, imewataka vijana wa waliopata mafunzo ya ujasiriamali na ujenzi wa vyoo bora kupitia mradi wa ushirikishwaji wa vijana katika ujenzi wa vyoo bora kibiashara (YESB), kuwa chachu ya mabadiliko kwenye jamii.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Maryprisca Mahundi, wakati wa kufunga mafunzo ya mradi unaotekelezwa na Shirika la Catholic Relief Service (CRS) na kushirikisha vijana 39 wa kata tatu za wilaya hiyo ambazo ni Sangambi, Chalangwa na Mbugani.

Aliwataka vijana hao kutumia elimu na ujuzi walioupata kuhamasisha jamii ya wananchi wa kujenga vyoo bora na kuvitumia ili kuepuka kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

“Kwenye ziara ambazo tumeanza za kuhamasisha ujenzi wa vyoo tumebaini familia nyingi hazina huduma hiyo, sasa ninyi mmepata mafunzo na mmejua umuhimu wa kuwa na vyoo, nendeni mkasaidie familia zenu kujenga na kutoa hamasa,” alisema Mahundi.

Alilipongeza CRS na wadau wengine wanaoshirikiana nao kwa kuanzisha mafunzo hayo ambayo alidai kuwa yatawasaidia vijana walioshiriki kupata ajira pamoja na kusaidia kutoa kuyaweka mzingira safi.

Ofisa wa Mradi wa YESB, Musa Mayage, alisema lengo la mradi huo ni kuwapatia ajira vijana hao ambao wengi wao wanatoka katika familia za kipato cha chini pamoja na kuisaidia jamii kujua umuhimu wa vyoo.

Alisema wakati wanaanza walitoa matangazo kwa ajili ya vijana hao kujitokeza na kwamba walijitokeza vijana 72 kutoka katika kata hizo tatu za Sangambi, Chalangwa na Mbugani, ambapo baada ya usaili walipungua na kubakia 45 lakini walioendelea wakawa 39.

Mayenga alisema vijana hao walipelekwa katika Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) cha Mbeya, ambapo walisomea masuala ya ujenzi wa vyoo hivyo kwa muda wa siku 21 kabla ya kurudi tena Chunya kwa ajili ya mafunzo ya ujasiriamali ya siku 10.

Alisema pia taasisi hiyo inashirikiana na taasisi zingine ikiwamo Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (Sido) ambalo linawaandalia vijana hao vifaa, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (Must) ambacho kinatoa ushauri wa kitaalamu.

Aidha, vijana hao waliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kuvipatia vikundi vyao mikopo ya asilimia nne ambayo huwa inatengwa kwa ajili ya kuwakopesha vijana kutokana na mapato ya ndani.

Akisoma risala ya vijana hao, Spora Edger, ambaye anatoka katika Kata ya Chalangwa, alisema wanakusudia kuandaa andiko la biashara ambalo wataliwasilisha katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kuomba uungwaji mkono.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli, aliwahakikishia vijana hao kuwa vikundi vyao vitapewa kipaumbele wakati wa utoaji wa mikopo kwenye vikundi vya wajasiriamali.

Aliwashauri vijana hao kuendelea kusambaza teknolojia waliyoipata kwenye kata zingine ambazo hazipo kwenye mradi ili kuwezesha wilaya nzima kuwa na teknolojia hiyo.