Wenye ulemavu kutosikia waomba maeneo biashara

22May 2020
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
Wenye ulemavu kutosikia waomba maeneo biashara

WATU wenye ulemavu wa kutosikia mkoani hapa wameiomba Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, kuwapatia maeneo yatakayowawezesha kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kujiingizia kipato ili kuondokana na utegemezi wa kuomba mitaani.

Ombi hili lilitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Japhary Gama, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu kutoka Chama cha Michezo cha Viziwi (DODSA), jijini hapa.

Akizungumza kwenye kikao hicho, mwenyekiti huyo ameiomba ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kuwapatia maeneo ambayo yatawawezesha kufanya shughuli mbalimbali ambazo zitakazowaingizia kipato, na hatimaye kuachana na dhana iliyojengeka ya kuonekana kuwa wao hawana uwezo wa kufanya kazi.

Gama, alisema kuwa kwa upande wao watu wenye ulemavu walio wengi wana uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali, changamoto waliyonayo ni kupata maeneo ambayo kwa upande wa jiji ndiyo wenye mamlaka ya kuwapatia.

“Wengi wetu hapa kati ya hawa wanachama wa chama cha michezo cha viziwi, wanauwezo wa kufanya kazi na

wakaweza kujitegemea kupitia kipato watakachokipata, hivyo tukiwezeshwa tunaweza kuondokana na dhana ya kutegemea wahisani,” alisema Gama.

Kwa upande wake ofisa masoko wa jiji hilo la Dodoma James Yuna, aliwataka watu hao wenye ulemavu wa kutosikia kuunda vikundi vya pamoja ili waweze kuwezeshwa na hatimaye wapatiwe maeneo ambayo yanayoweza kujipatia kipato kupitia fursa walizokuwanazo.

Yuna alisema ili watatuliwe changamoto walizo nazo kwa urahisi zaidi wanatakiwa kuungana kwa pamoja na kutoa kero zao ili waweze kusikilizwa na hatimaye kupatiwa maeneo.

“Kwa umoja wao walionao ofisi ya mkurugenzi inaweza kuwatatulia kero hiyo badala ya changamoto zao zikaletwa kwa mtu mmoja mmoja, fursa zipo ambao wao wanaweza wakapatiwa na kuwawezesha kufanya kazi ambazo zinazoweza kuwaingizia kipato bila kutegemea wahisani ukizingatia kuwa uwezo mnao wa kufanya kazi,” alisema Yuna.

Katika hatua nyingine ofisa huyo aliwataka watu hao wenye ulemavu kuendelea kujizatiti katika kujilinda na maambukizo ya ugonjwa wa corona kwa vitendo kulingana na hali waliyonayo.

Habari Kubwa