Wenye viwanda vya bia wafurahia ushirikiano

08Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Wenye viwanda vya bia wafurahia ushirikiano

MENEJA wa kiwanda cha kutengeneza bia TBL cha Dar es Salaam, Calvin Martin, amesema kuwa mafanikio ya viwanda vilivyo chini ya TBL Group nchini yanatokana na mikakati madhubuti iliyowekwa na kampuni mama inayomiliki viwanda hivyo ya SABMiller.

Meneja wa kiwanda cha kutengeneza bia TBL Dar es Salaam, Calvin Martin

Alisema uendeshaji wa viwanda hivyo unafuata miongozo, mikakati na sera za kampuni mama ya SABMiller, ambayo inaleta tija kwa kutekelezwa ipasavyo kwa kuwa ina mwelekeo wa uzalishaji unaolenga katika viwango vya kimataifa.

Meneja huyo alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wataalam wa fani mbalimbali wa Shirika la Maendeleo la Japan la (Jica), waliofanya ziara katika kiwanda cha kutengeneza Bia cha Dar es Salaam, kilichopo chini ya kampuni ya TBL Group.

Lengo la ziara yao ilikuwa ni kujifunza mbinu bora za uendeshaji viwanda zenye kuleta mafanikio, ambapo waliona hatua mbalimbali za uzalishaji wa vinywaji unaofanywa na kiwanda cha kutengeneza bia cha TBL na kuelezwa mikakati ya viwanda vilivyopo chini ya TBL Group hapa nchini ambavyo viko katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.

"Mafanikio yetu pia yanatokana na kujali maslahi ya wafanyakazi, utunzaji wa mazingira katika viwanda na maeneo vilipo viwanda, kuzingatia kanuni za mahesabu na kulipa kodi za serikali, kuzingatia kanuni za usalama kazini, taratibu za ajira na kuinua maisha ya watu wanaoishi maeneo vilipo viwanda ikiwamo kusaidia wazalishaji wa malighafi zinazotumiwa na viwanda vyake," alisema Martin na kuendelea:

"Miongozo ya kampuni mama ya SABMiller ikitumika popote na watumiaji kuizingatia lazima matokeo mazuri yapatikane na ndio maana viwanda vilivyopo chini ya TBL Group ni kioo cha sera ya uwekezaji nchini, kwani mbali na kuongoza kuchangia pato la serikali kwa kulipa kodi serikalini, kutengeneza ajira pia inanufaisha wananchi kwa njia mbalimbali na hii inatokana na kuwa na mfumo mzuri na utekelezaji wake kufanyika vizuri."

Martin aliuelezea ujumbe huo jinsi utekelezaji wa malengo ya SABMiller unavyofanywa na kampuni na jinsi yanavyoendelea kuiwezesha kupata mafanikio pia kunufaisha jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wao, wataalamu walijifunza mfumo na mwongozo wa uendeshaji viwanda kwa ufanisi wa SABMiller unaotumiwa na viwanda vyake ambao kitaalamu unaitwa Manufacturing Way, unaotoa miongozo bora na kanuni za uendeshaji viwanda zenye kuleta tija kuanzia kwa wafanyakazi hadi uzalishaji wa bidhaa bora zenye viwango vya juu vinavyokidhi mahitaji ya wateja kwenye masoko.

Kiongozi wa ujumbe huo, Isao Akilio, alipongeza mafanikio ya kampuni hiyo na kusema yanadhihirisha kuwa kanuni na miongozo bora ikifuatwa, uwepo wa viwanda bora unawezekana popote duniani hata katika nchi ambazo hazijaendelea kiviwanda kama ilivyo Tanzania na nchi nyingi za Afrika.

Habari Kubwa