WEZA yawawezesha wanawake tril. 1.5/-

22Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
WEZA yawawezesha wanawake tril. 1.5/-

WANAWAKE wa Zanzibar kwa miaka 4 wamefanikiwa kujiwekea akiba ya Sh. trilioni 1.5, jambo lililowawezesha kujiongeza kiuchumi, kimapato na ushindi kwenye vita ya umaskini.

Taarifa ya Asha Abdi Makame, Kaimu Mkurugenzi, Chama cha Wanawahabari Wanawake Tanzania (Tamwa Zanzibar), ilisema na kuongeza kuwa kukusanya akiba hiyo kulianza tangu Januari 2016 hadi Juni 2019.

Iliongeza katika jitihada za kuwasaidia na kuwainua wanawake wa Zanzibar, kinamama walihamasishwa kujiwekea akiba ya Sh. milioni 213, fedha zilizowekwa kuanzia mwaka 2016.

Kuanzia mwaka 2016 wanawake hao waliweza kujiwekea Sh. milioni 312 na ilipofika Juni 2019 kipato chao kiliongezeka kwa asilimia 80 na kufikia trilioni 1.5.

Awali wakati mradi unaanza wanavikundi walikuwa wakiweka akiba ya Sh. 250 kwa wiki, miaka miwili baadaye kwa kuwa kipato chao kilikua waliweka Sh. 3,800 hivyo kuanzia Januari hadi Juni waliweka Sh. 224,672,000, ilisema taarifa ya Tamwa Zanzibar.

Makame alisema Tamwa Zanzibar ikishirikiana na Milele Zanzibar Foundation (MZF) waliendesha programu maalum ya kukuza uwezo wa kiuchumi wa wanawake Zanzibar uliopewa jina la WEZA II ili kupunguza umaskini.

Dhamira kuu ya WEZA II ilikuwa ni kupunguza umaskini kwa wanawake na kuweza kusimamia masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku, ilisema taarifa ya Tamwa Zanzibar. Iliongeza kuwa vikundi 280 vyenye watu 6,000 vilifikiwa na kuhamasishwa ili kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini, kwanza kwa kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa (VSLs) na kufundishwa uzalishaji mali kwa ajili ya kujiongezea kipato (IGAs).

Ilisema mradi huo ulitekelezwa katika wilaya nane ambazo kwa upande wa Unguja ni Wilaya ya Kusini, Wilaya ya Kati, Kaskazini A na Kaskazini B, Pemba mradi wa WEZA II ulifanya kazi katika Wilaya za Wete, mkoani Chakechake na Micheweni.

Aidha, Tamwa Zanzibar imevihamasisha vikundi 24 vya kuweka na kukopa Unguja na Pemba kuanzisha miradi maalum ya kujiongezea kipato na kuvigawa vikundi hivyo katika kongano (clusters) nne za uzalishaji ambazo ni za wazalishaji wa vipodozi, mikoba, mboga na ufugaji wa kuku.

Kwa ujumla kuna kongano nane, nne Unguja na nne Pemba, vikundi hivyo tayari vimeshasajiliwa na pia vimepata vibali vya biashara na uzalishaji wa bidhaa kutoka mamlaka husika kama vile Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) na Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA), ilisema taarifa ya Tamwa.

“Katika ufuatiliaji wa harakati za wanawake kujikwamua kiuchumi, Tamwa Zanzibar, imegundua kuwa wanawake wengi hususan wa vijijini hawana mitaji ya kuwawezesha kufanya biashara wala kufanya shughuli za kilimo chenye tija, hivyo wanahitaji kusaidiwa kwa kupewa mikopo, ujuzi na vitendea kazi,” ilisema taarifa.

Kadhalika, wajasiriamali wadogo hupata shida kupata masoko ya bidhaa zao kwa sababu nyenzo zao za kujitangaza ni finyu. Mathalan hushindwa hata kushiriki katika maonyesho ya biashara kwa sababu hawawezi kulipia mabanda kwani banda hukodiwa kwa Sh. 200,000, alieleza Makame katika taarifa yake.

“Hivyo tunawashauri waandaaji wa maonyesho wawafikirie wazalishaji wadogo kwa kuwapunguzia gharama za kukodi mabanda,” aliongeza.

Wakati mradi wa WEZA II ukimalizika, hivi sasa Tamwa Zanzibar kwa kushirikiana na (MZF), inasimamia mwendelezo wa mpango huo wa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika mpango unaoitwa WEZA III ambao umejikita katika kuwaongezea uwezo wazalishaji kwa kuwapa mbinu za kujitegemea.

Walengwa wa mradi huo wako kwenye shehia 11 za Unguja Kaskazini A, Kusini na Magharibi na kwa upande wa Pemba Shehia 11 za Wete, Micheweni na Mkoani.

Habari Kubwa