Wiki 1 tani 100,000 mahindi zinunuliwe

07Sep 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wiki 1 tani 100,000 mahindi zinunuliwe

​​​​​​​CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa wiki moja kwa serikali kununua tani 100,000 za mahindi kutokana na baadhi ya wakulima wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kukosa masoko.

Aidha, kimezitaka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango, kujadiliana kuhusu kupunguza gharama ya mbolea kwa wananchi.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Alisema wakulima wamehamasika, wamelima kwa bidii na wajibu wa serikali ni kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika la mazao yao.

Chongolo aliongeza kuwa serikali ilitenga Sh. bilioni 14, kwa ajili ya kununua mahindi kwenye mikoa mbalimbali ya wakulima, lakini taarifa alizonazo fedha kwa sasa zimeisha.

“Taarifa tulizonazo kutoka kwa viongozi wa chama kwenye mikoa ambayo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), inanunua mahindi tumeambiwa fedha zimekwisha na sasa zoezi la kununua linasuasua, tukasema hatuwezi kukaa namna hii, wakulima wetu wana mahindi hawana sehemu ya kuuza.

“Maagizo yetu kwa serikali watafute fedha wanapojua na zoezi la kununua mahindi liendelee kwenye maeneo yote, ambayo tulikubaliana mahindi yaendelee kununua, hadi sasa tunaambiwa wamenunua wastani wa tani 25,000 -28,000 na sisi CCM tunaagiza wanunue tani 100,000,” alisema.

Pia, alisema taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) inaonesha kuwa mwaka huu kutakuwa na tatizo la mvua hazitanyesha kwa kiwango chenye tija na hivyo kutishia mwaka ujao kuwapo na uhaba wa chakula.

Akizungumzia kuhusu uchache wa vituo vya kununulia mahindi, alitaka NFRA watakapoanza kutekeleza agizo la kununua tani hizo za mahindi kusogeza vituo vya kununulia, ili kuwaondolea adha ya usafiri wakulima.

“Kuna malalamiko hii Sh. 500 kwa kilo wamekuwa wakikatwa sehemu ya fedha kwa madai kuwa ni ya usafiri, hii  ni kumuonea mtu anayeishi mbali na mjini, CCM inasema mtu aliyepo eneo lolote mahindi yanunuliwe kwa bei hiyo, ili kuwa na bei sawia kwa wakulima wote na suala la usafiri lisiwe mzigo kwa wakulima,” alisema.

Alisema Sekretarieti ya CCM itakwenda kwenye mikoa hiyo baada ya wiki moja kuangalia utekelezaji wa maagizo iliyotoa kwa kununua mazao bila masharti.

Kuhusu mbolea, alisema bei imepanda kwa kiwango kikubwa nchini na CCM iliahidi kuwalinda wakulima, licha ya tatizo hilo kuwa la dunia na kuagiza serikali kupitia wizara zake wakae waanze kujadiliana namna ya kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi.