Wito kutumia nishati rafiki kwa mazingira

05Jul 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Wito kutumia nishati rafiki kwa mazingira

KAMPUNI ya usambazaji wa huduma za vifaa vinavyotumia umeme wa nishati ya jua (Mobison), imewaomba Watanzania kutumia nishati zinazotunza mazingira.

Akizungumza katika Maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara (DTIF) Mkuu wa Kitengo cha Usambazaji Mobisol, Francis Shenyagwa, alisema ni muda mwafaka kwa Watanzania kuanza kuwa na mtazamo chanya kuhusiana na manufaa ya muda mrefu yanayotokana na matumizi ya nishati ya jua.

Alisema umeme wa jua ni chanzo kinachofaa cha nishati mbadala majumbani na nchi nyingi tayari zimegundua ukweli na zimeachana na vyanzo vya kuzalisha nishati ya umeme vilivyozoeleka kama makaa ya mawe.

"Sisi Mobisol tunaitambua haja hiyo, na ndiyo maana tumeingiza sokoni mifumo inayokwenda mbali zaidi ya ile ya kukidhi haja ya upatikanaji wa mwanga majumbani tumekuja na vifaa ambavyo vinakidhi haja nyingi ambapo bidhaa zetu ni bora ikilinganishwa na vile vinavyotumiwa majumbani kwenye maeneo ambayo hayana umeme, kama mshumaa na taa za chemli," alisema Shenyangwa.

Shenyagwa alisema wapo nchini kwa zaidi ya miaka minne sasa hivyo wanahakikisha huduma wanayotoa inakidhi mahitaji ya Watanzania na kuwafikia watu wanaoishi katika maeneo ya ndani hususani mashamba yasiyofikika kwa urahisi.

"Sisi ni wadau wa maendeleo wa kudumu nchini Tanzania kwenye jitihada za kufikisha huduma za umeme unaotokana na nguvu ya jua kwa maeneo yasiyokuwa na umeme, na tupo tayari kuwekeza zaidi katika kupanua wigo wa huduma zetu,” alisema na kuongeza:

“Dhamira yetu ya kusambaza umeme wa jua katika kila sehemu nchini inajidhihirisha wazi kwa jinsi ambavyo tumekita shughuli zetu hadi maeneo mengi ya mashambani, ambapo kipato ni cha msimu na kufanya malipo kutoka kwa wateja yawe ni ya kusuasua.”

Alisema bado kuna mambo ya ziada yanayostahili kufanywa ili kujenga usimamizi dhabiti wa soko la bidhaa zinazotumia umeme wa jua ili kuhakikisha kuwa wateja wanapata bidhaa bora.

"Tunaishauri serikali iende hatua ya mbali zaidi katika usimamizi wa soko la bidhaa zinazotumia umeme wa jua, ili kuhakikisha kuwa walaji wanajipatia thamani halisi ya pesa yao," alisema Shenyagwa.

Habari Kubwa