Wizara sasa yageukia chuma,makaa ya mawe

20Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
 LUDEWA
Nipashe Jumapili
Wizara sasa yageukia chuma,makaa ya mawe

WIZARA ya Madini imesema itashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kuweka msukumo kuhakikisha  miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na ule wa Chuma Linganga inaanza kutekelezwa.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto), akiongozwa na Meneja wa mgodi wa Makaa ya Mawe TANCOAL, David Kamenya (wa pili kulia), kutembelea maeneo ambapo uchimbaji wa makaa hayo unafanywa katika machimbo yaliyopo Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma juzi. PICHA: WIZARA YA MADINI

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, alisema hayo juzi  wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za madini mkoani Njombe na kuona namna ya kutatua changamoto  zinazohusu wizara  katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema miradi hiyo ni ya kimkakati ambayo taifa linatarajia kunufaika kwa kiasi kikubwa, hivyo kutokana na umuhimu wake, wizara itashirikiana na wizara hiyo kupitia NDC kuhakikisha hatua zaidi zinapigwa ili hatimaye ianze kutekelezwa kwa kuwa imechukua muda mrefu.

Nyongo alisema miradi hiyo ni mikubwa ambayo taifa linatarajia kunufaika nayo  kupitia ajira  na kuongeza pato la taifa huku akiyataja madini ya chuma kuwa  moja ya malighafi muhimu kwa uchumi  wa Tanzania ya viwanda.

Alisema serikali ina imani kubwa  kuwa  miradi hiyo itaanza huku  ikitegemea  kupeleka  maendeleo  kwa wananchi kupitia miradi husika.

 “Wizara yetu ndiyo inatoa leseni za madini na tayari tulishatoa leseni ya makaa ya mawe Mchuchuma kwa hiyo nimefika kuangalia changamoto ambazo ziko upande wa wizara yetu ili kuzitatua tutoke hapa. Miradi hii tumeisikia miaka mingi, hivyo ni wakati sasa tunataka ianze.” alisisitiza Nyongo.

Naibu waziri alisema ikiwa wizara ndiyo inatoa leseni za madini,  inao wajibu wa kujua yule aliyepewa leseni kama anaifanyia kazi na kuongeza.

“Sisi tuliotoa leseni lazima tuangalie tuliyempa leseni amekwama wapi  lakini pia tujue  miradi hii inaanza lini? Makaa ya mawe na chuma vyote vinahitajika kwa taifa. Tunatambua makaa ya mawe ni madini ambayo yana tija kwa uchumi kwa nchi,” alisema.

Nyongo pia alisema mradi wa makaa ya mawe unatarajiwa kuzalisha umeme ambao mbali na kuuza kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), umeme huo unatarajia kutumika katika kuzalisha madini ya chuma Liganga.

 “ Mpango ni Liganga kutumia megawati 250 kwa shughuli zake za kuzalisha chuma na megawati 350 zitauzwa Tanesco kuzalisha umeme,” aliongeza.

Alisema kuchelewa kwa miradi hiyo kumetokana na changamoto za kimkataba ambazo bado ziko katika majadiliano katika ngazi za juu na kuitaja baadhi ya mikataba hiyo kuwa ni  pamoja na mikataba ya upunguzaji wa kodi.

Kuhusu fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo, alianza kwa kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Ludewa kwa kutenganisha suala la miradi hiyo na fidia  na kwamba  taratibu za juu zikikamilika, wananchi watalipwa fidia, hivyo kuwataka kuwa na subira na kuwa tayari kupisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Awali,  Mkuu wa Mkoa wa Njombe , Christopher Ole Sendeka alimweleza naibu waziri umuhimu kwa Wizara ya Madini kujielekeza kupata taarifa halisi kuhusu utafiti mbalimbali uliofanyika awali kuhusu  akiba iliyoko ya madini ya chuma  Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma.

Habari Kubwa