Wizara kuboresha masoko ya samaki

17Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wizara kuboresha masoko ya samaki

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeanza mpango kabambe wa kufufua, kujenga na kukarabati mialo na masoko yote ya samaki nchini kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa ajili ya kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi.

Mpango huo wa uboreshaji wa mazingira hayo ya shughuli za uvuvi yameanzia kwenye Soko la Kimataifa la Samaki la Magogoni Feri jijini Dar es Salaam, serikali iktenga takribani Sh. bilioni mbili kulifanyia ukarabati mkubwa wa miundombinu yake na kupanua wigo mpana zaidi wa biashara za kimataifa.

Wizara hiyo pia imeingia mkataba na Mshauri Mwelekezi M/S Inter Consult Ltd kwa ajili ya kutayarisha michoro na makadirio ya ukarabati wa soko hilo na imeshampata mzabuni kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo na kazi hiyo itaanza hivi karibuni.

Akitangaza mpango huo wa uboreshaji wa mialo na masoko ya samaki kote nchini sambamba na kukabidhi vyoo vipya vya kisasa vyenye matundu 12 vilivyojengwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Manispaa ya Ilala Dar es Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema serikali imekataa wavuvi na shughuli za uvuvi kudharauliwa.

Waziri Mpina alisema jengo hilo jipya lililojengwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, lina uwezo wa kuhudumia watu 40 kwa wakati mmoja, hivyo kukamilika kwa vyoo hicho ni hatua madhubuti ya kuboresha afya za watumiaji wa soko hilo wakiwamo wavuvi, wachakataji wa samaki, mama lishe, wanunuzi wa samaki na wadau wengine.

Waziri Mpina alisisitiza kuwa kwa miaka mingi sasa wavuvi na shughuli za uvuvi wamekuwa wakidharauliwa na kutopewa msukumo wowote na kwamba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imekuja kuwafuta machozi.

Alitoa miezi mitatu kwa halmashauri zote kuboresha mialo na masoko yote nchini na kueleza kusikitishwa kwake na tabia iliyojengeka ya baadhi ya halmashauri kugeuza mialo na masoko kuwa chanzo cha mapato ya halmashauri na kushindwa kuboresha miundombinu yake, hasa vyoo na kutotekeleza Sheria za Uvuvi Namba 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009.

Mpina alisema wizara imekamilisha kazi ya ujenzi na kukabidhi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, akimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wake kuhakikisha mradi huo unasimamiwa, kutunzwa na kutumika kama ilivyokusudiwa.

Pia alimwagiza Katibu Mkuu (Uvuvi) kuandaa na kusambaza miongozo ya usimamizi wa masoko na mialo kwa wadau na halmashauri zote nchini ifikapo Februari Mosi, mwaka huu, ili kuweka masharti ya uendeshaji na usimamizi makini wa shughuli za uvuvi.

Aliipongeza menejimenti ya soko hilo kwa hatua ya kupunguza matumizi kutoka Sh. milioni 100 hadi kufikia milioni 73 kwa mwezi tangu walipopokea maelekezo yake aliyoyatoa mwaka jana.

Katibu Mkuu, Rashid Tamatamah, alisema mradi wa vyoo hivyo umegharimu Sh. milioni 163 na kwamba utapunguza adha kwa wananchi wanaotumia soko hilo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Makwiro, alimshukuru Waziri Mpina kwa uamuzi wa wizara kujenga vyoo hivyo na kumhakikishia kuwa kama serikali ya wilaya itasimamia miundombinu hiyo ili idumu kwa miaka mingi.

Habari Kubwa