Wizi NBC Moshi: Tanzania ‘yabanwa’ Mahakama ya Afrika

20Mar 2016
John Ngunge
Arusha
Nipashe Jumapili
Wizi NBC Moshi: Tanzania ‘yabanwa’ Mahakama ya Afrika

MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imeiamuru serikali kuharakisha na kumaliza kesi zilizoombwa na walalamikaji Wilfred Onyango Nganyi na wenzake tisa.

Aidha, AfCHPR imetoamiezi sita kwa upande wa walalamikiwa (Tanzania) kutelekeza maagizo ya malalamiko ya walalamikaji.

Onyango na wenzake raia wa Kenya walikamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za kuiba kwa kutumia silaha zaidi ya Sh.

bilioni 5 kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la Moshi, Mei 21, 2004 na mauaji Benedict Mfuria Julai 26, 2005.
Watuhumiwa hao walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ambako walifungwa miaka 30 lakini wanakabiliwa na kesi nyingine ya mauaji namba 10 ya mwaka 2006 iliyopo Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hukumu hiyo iliyosomwa na Jaji Gerard Niyungeko mbele ya majaji wenzake wanane, iliamuru Serikali ambaye katika kesi hiyo ni mlalamikiwa kuhakikisha inaharakisha na kumaliza kesi za rufani za waombaji hao katika mahakama za nchini.

Pia mahakama hiyo imemtaka malalamikiwa kutoa msaada wa kisheria kwa walalamikaji kwa kesi ambazo wamefungua katika mahakama za ndani.

Mlalamikiwa pia ameamuriwa kuitaarifu mahakama hiyo kuhusu hatua alizochukua kutekeleza maagizo aliyopewa ndani ya miezi sita baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Aidha Jaji Niyungeko, alimwelekeza malalamikaji kufungua maombi ya kudai fidia ndani ya siku 30 na kwa upande wa mlalamikiwa kujibu maombi hayo kwa muda huo huo wa siku 30.

Mapema mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi ziliombwa na mlalamikiwa akiitaka mahakama hiyo itupilie mbali shauri hilo kwa kuwa haina mamlaka kisheria ya kuisikiliza.

Katika maombi ya shauri lao namba 006/2013 mahakamani hapo, Onyango na wenzake, walidai walikuwa nchini Msumbiji wakitafuta fursa za kufanya biashara wakati walipokamatwa Januari 16, 2006 na kusafirishwa kwa ndege ya kijeshi chini ya ulinzi hadi nchini ambako waliwekwa rumande.

Walisema baadaye walifunguliwa mashtaka ya mauaji na mashtaka matatu ya wizi wa kutumia silaha.
Washtakiwa hao walilalamikia kesi yao kuchukua muda mrefu huku ikiahirishwa mara kwa mara na walikosa msaada wa kisheria.

Pamoja na mambo mengine, walilalamikia pia kupata mateso, unyanyasaji na kupigwa na polisi na kufungwa jela kinyume cha haki za binadamu.

Mwanasheria wa serikali, Mark Mulwambo, alisema
watatekeleza amri ambazo wamepewa na mahakama hiyo.

Kwa upande wake wakili kutoka Chama cha Wanasheria wa Afrika (PALU), Evelyn Chijarira na wenzake Abiha Kasmani na Amandine Rushenguzimega, walitaka nchi wanachama kuheshimu haki za binadamu wanapowakamata
watuhumiwa na kuendesha mashauri yao kwa misingi ya hiyo.

Habari Kubwa