Yaelezwa CCM si chaka la wakwepa kodi, waovu

03Sep 2017
Cynthia Mwilolezi
Nipashe Jumapili
Yaelezwa CCM si chaka la wakwepa kodi, waovu

KATIBU wa CCM Mkoa wa Arusha, Ernest Mpanda, amewaonya wanachama wapya kuwa wasidhani chama hicho ni kichaka cha wasiolipa kodi au kufanya mambo yasiyofaa.

KATIBU wa CCM Mkoa wa Arusha, Ernest Mpanda.

Aidha, amesema mtaji wa CCM ni wanachama na kutoa rai kwa wapya kuhakikisha wanaisoma na kuielewa ilani ya chama chao.
Mpanda aliyasema hayo wakati akiwapokea wanachama wapya wafanyabiashara zaidi ya 860 kutoka Stendi Ndogo, Soko la Kilombero pamoja na Ranger Safari.

Alisema CCM si kichaka cha wanaokula rushwa au kufanya mambo yasiyofaa na kusisitiza kuwa ule wakati wa watu kupanga safu ya wagombea umepitwa na wakati na atakayebainika atachukuliwa hatua.

"Kukiri upungufu si kujidhoofisha bali ni kujirekebisha na tumejitathimini tulipotoka, tulipojikwaa na sasa hivi tupo wapi maana hivi sasa tuna CCM mpya ndiyo maana tumedhamiria kujijengea chama chetu kwa misingi ya usawa, uhuru na haki "

Aliwaomba kumwombea Rais John Magufuli ili kuleta maendeleo ndani ya chama na nchi yetu kwani hivi sasa mambo yanayofanywa na Rais Magufuli ni ya kimaendeleo na yenye kuleta heshima kwa nchi ..

Katibu wa Soko la Kilombero, Ramadhani Ayubu, alisema wameamua kujiunga na CCM kutokana na spidi ya utendaji kazi wa Rais Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia.

Alisema wamejiunga na CCM kwani awali walipokuwa Chadema waliambulia vurugu zisizo na tija badala ya maendeleo.

Mwanaccm ambaye awali alikuwa Chadema, Aneth Minja, alisema amerudi kwani giza na nuru havichangamani.

Habari Kubwa