Z’bar yajipanga utalii kuimarika Pemba

21May 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Z’bar yajipanga utalii kuimarika Pemba

SERIKALI ya Zanzibar imesema imejipanga kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika katika kisiwa cha Pemba na kukuza uchumi wa taifa na pato la wananchi kwa ujumla.

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo:PICHA NA MTANDAO

Hayo yalisemwa na Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, wakati akifanya majumuisho na kujibu hoja za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2020-2021.

Alisema tayari serikali imetangaza utalii kwa wote kwa lengo la kuwanufaisha wananchi na kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

Alisema serikali inakusudia kuliimarisha eneo la Kaskazini ya Micheweni kuwa moja ya kivutio cha watalii kwa kujenga hoteli kubwa za kitalii.

Alikiri kuwa sekta ya utalii imechelewa kuimarika katika kisiwa hicho kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ukosefu wa miundombinu ya umeme na barabara.

“Tunawataka wananchi wa kisiwa cha Pemba kujipanga na kujitayarisha kuupokea utalii ambao miongoni mwa faida zake kubwa ni kukuza pato la wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisema.

Vile vile, Kombo alikemea na kuwataka wananchi kuacha kuuza maeneo yao ya vijijini ikiwamo yaliopo pembezoni mwa fukwe za bahari kwa wawekezaji na watu wanaotaka kumiliki maeneo hayo kwa shughuli za utalii.

Alisema njia nzuri na ushauri wa serikali ni kuingia ubia na watu wanaoyataka maeneo hayo kwa ajili ya kujenga hoteli za kitalii na mradi huo utaendeshwa kwa njia ya ubia.

“Ukiingia ubia katika jengo la hoteli iliyojengwa maana yake wewe utafaidika na hisa iliopo pale katika muda wote wa maisha yako na ukifa itafaidika familia yako hadi watoto,” alisema.

Baadhi ya wananchi waliochangia bajeti hiyo waliitaka serikali kuhakikisha kwamba utalii unadumisha utamaduni na silka za wananchi.

Mwakilishi wa Jimbo la Chakechake, Suleiman Sarahani, alisema wananchi wa Pemba wapo tayari kuupokea utalii baada ya kuimarika kwa miundombinu mbalimbali ikiwamo barabara na umeme hadi vijijini.

“Wananchi wa Pemba wanaisubiri serikali na sekta binafsi kufungua milango ya sekta ya utalii kwa ujenzi wa miradi ya hoteli ili wananchi wafaidike kwa kuuza bidhaa zao mbalimbali na kupata fedha,” alisema.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa jumla ya Sh. 20,389,800,000, kati ya hizo Sh. 14,289,800,000 kwa kazi za kawaida na Sh. 6,100,000,000 kwa kazi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 

Habari Kubwa