Zaidi ya vijana, wanawake 400 wapatiwa mikopo

19May 2017
Godfrey Mushi
Nipashe
Zaidi ya vijana, wanawake 400 wapatiwa mikopo

ZAIDI ya wanufaika 446 ambao ni makundi ya vijana na wanawake katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha, wamepatiwa mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 75, licha ya kuwapo madai kwamba wengi wao hawakopesheki.

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu, jana aliiambia Nipashe kwamba kati ya wanufaika hao, vikundi 20 ni vya wanawake 316 waliochukua asilimia tano ya fedha zinazotengwa na halmashauri katika makusanyo ya ndani.

“Vijana wao wamewezeshwa kupitia vikundi saba vyenye wanufaika 130, lakini waliobaki ni wanawake ambao ndio wengi zaidi wanajitokeza,” alisema.

Aliyataka makundi yaliyopewa fedha hizo kuzirejesha kwa wakati ili kusaidia vikundi vingine kunufaika kiuchumi na fungu hilo ambalo linatengwa na Halmashauri ya Siha.

Taarifa za baadhi ya Halmashauri za mkoa wa Kilimanjaro, zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya vijana wasio na ajira hawakopesheki kutokana na mwamko mdogo wa kujiunga kwenye vikundi, huku wanaopewa mikopo ya fedha wakishindwa kupeleka marejesho.

Hali hiyo inadaiwa kuchangia vijana wengi wasio na ajira kuendelea kusota vijiweni na kuilalamikia serikali.

Fedha hizo ni asilimia tano inayotengwa na halmashauri kupitia makusanyo ya ndani kwa ajili ya kusaidia uibuaji wa miradi ya
kiuchumi ya vijana na wanawake.

Akitoa ufafanuzi wa fedha hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Valerian Juwal, alisema kama idadi kubwa ya vijana na wanawake hawatakubali kusukumwa na kutumia vizuri mikopo yao ni

dhahiri watajikwamua kiuchumi na kuacha kukaa vijiweni au kujiingiza kwenye matumizi au biashara ya dawa za kulevya.

 “Nataka niwape somo vijana na wanawake mnaonufaika na fedha hizi, tambueni kwamba siyo za kufanyia anasa ni za kufanyia kazi zitakazowawezesha kuingiza kipato kitakachobadili maisha yenu,” alisisitiza.