Zanzibar kuanza uvuvi bahari kuu

05Dec 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Zanzibar kuanza uvuvi bahari kuu

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeahidi kujikita katika uwekezaji wa uvuvi wa bahari kuu pamoja na kujenga viwanda vya kuchakata mazao (kusarifu), ya baharini ili yalete tija katika mabadiliko ya uchumi wa bahari.


Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Hassan Khamis Hafidh, picha mtandao


Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Hassan Khamis Hafidh, wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Tumbe Omar Seif Abeid, aliyetaka kujua serikali imejipanga vipi katika kuwawezesha wavuvi kuvua bahari kuu.

Hafidh alizitaja juhudi zilizoanza kuchukuliwa na serikali ikiwamo kununua boti ya uvuvi ya Sehewa 2 ambayo itakuwa inavua kwenye maji ya bahari kuu.

Alisema uvuvi wa bahari kuu umechelewa kuanza kufanyiwa kazi na kutoa huduma kufuatia kukosekana kwa vyombo vya uvuvi vyenye uwezo wa kuyafikia maeneo hayo.


“Mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha wavuvi wanavua katika maeneo ya bahari kuu kwa ajili ya kupata mavuno mazuri ya samaki,”alisema.


Alieleza kuwa wapo aina ya samaki kama jodari ndiyo wanaopatikana kwa wingi katika bahari kuu ambao bado hawajavuliwa kwa ajili ya kupata tija kiuchumi na maendeleo.

“Jodari wanapatikana katika maeneo ya bahari kuu ingawa bado hawajavuliwa kwa sababu wavuvi wetu hawayafikii maeneo hayo,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa juhudi zimeanza za kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vya kusarifu mazao ya baharini ikiwamo mwani.

Alisema wananchi wengi wamehamasika kulima kilimo cha mazao bahari, lakini hadi sasa bei ya mwani ni changamoto kwani ni ndogo kiasi cha ya kuwavunja moyo wakulima wa kilimo hicho.


“Yapo matumaini makubwa ya kujengwa kwa viwanda vya kusarifu mazao ya baharini ikiwamo mwani hatua ambayo italeta mabadiliko makubwa ya maendeleo ya kilimo hicho na mavuna ya maliasili zinazotokana na bahari,” alisema.

Habari Kubwa