Zanzibar kukopa Dola milioni 33 kuimarisha kilimo mpunga

14May 2022
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Zanzibar kukopa Dola milioni 33 kuimarisha kilimo mpunga

SERIKALI ya Zanzibar imesema imejipanga kuinua kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula na inakusudia kukopa Dola milioni 33 za Marekeni katika taasisi za fedha za kimataifa.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema hayo jana  katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hoja zilizoibuliwa na wajumbe kuhusu maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji cha mpunga.

 

Dk. Mohamed alisema serikali inakusudia kukopa Benki ya Dunia Dola milioni 15 ambazo zitatumika katika kuimarisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.

 

Pia alisema alisema serikali inakusudia kukopa kupitia Benki ya Exim Dola milioni 18 ambazo zitatumika katika uimarishaji wa kilimo cha mpunga ambacho kitahusisha utoaji wa wa elimu kwa mabibi shamba na mabwana shamba vijijini Unguja na Pemba.

 

Alibainisha kuwa fedha hizo zitatumika katika kuimarisha hekta 1,000 za mpunga katika mabonde 10 Unguja na Pemba hatua ambayo imelenga kuongeza uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji maji.

 

''Mheshimiwa Spika hiyo ndiyo mikakati ya Serikali ya Mapinduzi katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji hatua ambayo inakwenda sambamba na mikakati ya kujitosheleza kwa chakula,” alisema.

 

Alisema hayo ni maelekezo ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye  mikakati yake inayotokana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, imejikita  katika kujitosheleza kwa chakula.

 

Kilimo cha umwagiliaji, alisema kimeshuka uzalishaji wake kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mabadiliko ya tabianchi ambayo yamefanya kupungua kwa mahitaji ya mvua.

 

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walitishia kuzuia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji baada ya kudai kwamba uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji cha mpunga haukupewa kipaumbele katika mwaka ujao wa fedha.

Habari Kubwa