Bomoabomoa Mkwajuni ilivyompora malighafi inayomuweka mjini

22Jan 2016
Mary Geofrey
Nipashe
Bomoabomoa Mkwajuni ilivyompora malighafi inayomuweka mjini

BOMOABOMOA imepita katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na wakazi wanaokadiriwa 1,000 wameathirika.

Lakini, mchonga viatu vya matairi, Joseph Chimli (25) naye ni muathirika anayeonja kwa namna yake, kwani bonde la Kinondoni Mkwajuni, ndilo linalomuweka mjini kimaisha, hata akafikia hatua ya kimiliki nyumba mkoani Dodoma.

Anaeleza kuwa shughuli anazozifanya katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, hasa gereji za magari ambako matairi yanapatikana.

Chimli anaeleza kuwa, katika bonde la Kinondoni Mkwajuni, alikuwa akifanya shughuli zake mara tatu kwa mwezi na anongeza:

"Katika maeneo ambako ni rahisi kwa shughuli zangu, ni hapa na nimekuwa nikifika kwa sababu nakuta matairi yamekusanywa na mimi naanza kuchonga."

Anasema kuwa, vitendea kazi pekee anavyobeba katika harakati zake bondeni Kinondoni Mkwajuni ni kisu na tupa ya kunolea kisu na mfano wa kandambili inayotumika kumpatia saizi ya viatu.

"Kwanza hapa kuna kivuli, nikifika nakaa chini naanza kuchonga matairi ambayo nayakuta hapa na wale walionikusanyia nawapa fedha kidogo.

"Pia naendelea na shughuli zangu taratibu wakati nikipiga stori na washikaji zangu na jambo lingine ni kuwa sehemu salama," anasema Chimli.

CHANGAMOTO

Anasema kuwa kutokana na shughuli anayoifanya, analazimika kuwa mchafu wakati wote. Anafafanua:"Kwa kazi hii siwezi kuwa msafi, nachafuka sana marangi meusi ya matairi, wananchi wananiona kama chizi."

Mchonga viatu huyo anafafanua kuwa, anashindwa kueleweka ndani ya jamii anayokutana nayo, akiwa ndani ya daladala na anavyokatisha mtaani.

Chimli anafafanua kuwa maisha ya fani yake kuwa inamkwaza hata kupata mwenza wa maisha yake, kwani amekuwa mchafu na baadhi yao wamekuwa wakimcheka.

"Ukimsalimia mwanamke anakuona kama chizi uliyekosea njia lakini pia nikiwa nimeoga wamekuwa wa kwanza kuniomba fedha za chips.

"Jambo hili linaniumiza sana ikizingatiwa kuwa natamani kuwa na mwanamke anayenipenda na kuipenda kazi yangu," anasema Chimli katika kauli ya masikitiko.

Anaongeza kwamba, hatarajii kuiacha kazi hiyo ambayo kwa sasa anaimudu, kuipenda na kuijali mno.

CHANGAMOTO

Anainisha changamoto anayomkabili baada ya bomoabomoa, ni kwamba matairi yametoweka anakofanyia kazi, wakati zamani alikuwa akiyakuta na anafanya kazi akibadilishama mawazo na washikaji katika eneo lake la kazi .

Kutokana na hali hiyo, Chimli analalamika kukabiliwa na kazi ya ziada ya kuokota matairi yaliyotuama kwenye maji, hali iliyo tofauti na mazingira ya zamani, pia sasa ana hofu kubwa ya usalama wake.

"Kama unavyoona dada hili bonde ni hatari sana. Liko kimya, vibaka ndio makazi yao kwa hiyo huenda nikafanyiwa jambo lolote kwa sababu watu ninaowafahamu sipo nao tena," anasema.

MAGUMU ALIYOPITIA

Chimli anaelezea namna alivyopambana na ugumu wa maisha na kujijengea heshima kwa familia na ndugu wanaomzunguka, kabla ya kuanza kuchonga viatu vya matairi.

Chimli ambaye kupata elimu ya shule ya sekondari, anasema kuwa alianza maisha kwa kulala katika soko la Buguruni, jijini Dar es Salaam, kutokana na kukosa makazi ya kuishi.

Anasema, jitihada za kupambana na maisha, zilimuwezesha kuruka kiunzi hadi leo hii kuwa na hadhi ya baba wa mtoto mmoja mwenye miaka minne na mmiliki wa nyumba ya vyumba vitatu.

Chimli ambaye ni mzaliwa wa mkoa wa Dodoma, anasema alipitia maisha magumu ya kutoka mkoani kwao kwa ushawishi wa rafiki yake, kwenda jijini Dar es Salaam kwa shughuli ya kuuza maji.

"Rafiki yangu alikuja Dodoma mwaka 2007 akanichukua nije nifanye shughuli ya kuuza maji. Nilifikia kwake na kuanza kazi hiyo kwa muda wa miezi mitatu," anasema.

Chimli anasema kuwa, wakati akiendelea na shughuli hiyo alipoteza kaka yake aliyefariki na kulazimika kwenda msibani kwa takriban siku tano.

anasema, aliporudi alikokuwa akikaa Buguruni na familia ya rafiki yake huyo, alikuta wamehama.

"Nilishangaa sana nilipohoji waliniambia wameondoka kwa sababu wanadaiwa mkopo waliokuwa wamekopa SACCOS, hivyo wakaamua kutoroka.

"Nilichukua nguo zangu zilizokuwa zinaning'inia juu ya kamba nikaanza maisha mapya," anasema Chimli.

Anasimulia mkasa huo kwamba hakuwa rahisi kuamini kilichotokea, kwani aliona mwelekeo wa maisha yake yamekabiliwa na kikwazo kikubwa, kwani hakuwa na ndugu jijini Dar es Salaam.

AHAMIA KULALA SOKONI

"Nililazimika kulala soko la Buguruni kwa muda wa mwezi mmoja, nikaanza kuokota na kuziuza chupa za maji huku nikiambulia fedha ya kula pekee," anasema.

Chimli anasimulia zaidi kuwa, biashara hiyo ndiyo ilikuwa inampatia kipato kidogo, kwani alikuwa akiuza kilo moja ya chupa kwa Sh. 200 hali ambayo hakuridhika nayo.

Anafafanua kuwa, baadaye aliamua kubadilisha mfumo wa biashara kwa kuanza kuuza chupa zilizo na ubora ambazo ni za juisi, wateja wake wakiwa ni wanatengeneza kinywaji hicho.

"Nilikuwa natembea umbali mrefu natafuta chupa, naziosha na kuziuza kwa wauza juisi kwa moja Sh. 30 kwa chupa moja na kidogo nikaanza kuongeza kipato," anasema.

Anasema wakati akiwa bado analala sokoni Buguruni, aliamua kujiunga na kikundi cha sanaa, ili kujiepusha na vishawishi vya kutumia dawa za kelevya.

"Kuna rafiki yangu aliniunganishia kwa baba mmoja ambaye alikuwa na duka, nikawa ninalala pale badala ya sokoni, lakini bila ya malipo yoyote," anasema.

Chimli anasema kuwa, wakati akiendelea kulala katika eneo hilo, marafiki zake walianza kwenda eneo hilo kuchonga viatu vya matairi ya magari.

"Kwa sababu nilikuwa naaminika kwa yule mwenye duka, marafiki zangu walikuja kuomba kukaa nje ya duka langu, wakawa wanafanya shughuli za kuchonga viatu vya matairi," anasema.

Chimli anasema kuwa baada ya muda mfupi, aliyekuwa akifanya shughuli hizo alipata ofisi, ambako naye akamfuata kwenda kujifunza ufundi huo.

"Kutokana na biashara kuchanganya nililazimika kujituma na kukaa naye karibu japo alikuwa ananitumikisha, lakini lengo langu na mimi kupata ujuzi.

"Kama wahenga wanavyosema mtafutaji hachoki, nikavumilia masumbufu ya kutumwa kuambiwa nifagie uwanja kila siku," anasema.

Chimli anasema, baada ya kupata ujuzi ndipo alipopata mtaji wa sh.30,000 akishirikiana na rafiki yake aliyempa mtaji wa kununua vifaa.

"Tulianza kuchonga viatu hivi na ndani ya wiki mbili tulimaliza biashara na kupata Sh. 200,000. Tuligawana faida na kuendelea na kazi, tulikuwa tukishirikiana mmoja anavipeleka sokoni na mwingine anandaa mzigo," anasema.

Baada ya muda mfupi, aliamua kujitegemea kwa kuuza viatu vyake kwa bei ya Sh.700 kwa ndala moja isiyokamilika na wateja wao walinunua na kuziweka kamba, kisha wakaviuza kwa bei ya Sh. 2,000.

MAFANIKIO

Chimli anasema, hivi sasa amefanikiwa kuwa kuwa na wateja kutoka nchi jirani ya Msumbiji, kwani wafanyabiashara wa mipakani wanazichukua na kwenda kuziuza huko.

Anasema kipato chake cha sasa ni Sh. 400,000, huku akielezea kasi yake ya kazi ni uwezo wa kuchonga viatu zaidi ya 200, biashara inayomfanya aishi maisha ya amani.

Mjasiriamali huyo anayekiri ujasiriamali wake kukumbwa na mtihani mzito kutokana na bomoabomoa, lakini kipato chake hadi sasa hakijatetereka.

Habari Kubwa