Bomoabomoa yaliza Wachina Mikocheni

02Jan 2016
Nipashe Jumapili
Bomoabomoa yaliza Wachina Mikocheni

BIASHARA ya gereji ya Wachina ni moja ya nyumba 600 zilizowekwa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa kabla ya keshokutwa, katika eneo la Mlalakuwa, Mikocheni jijini Dar es Salaam kutokana na kujengwa ndani ya eneo la hifadhi ya mto.

Gereji kubwa na maarufu ya Spring City Enterprises iliyopo ndani ya mita 60 kutoka bonde la mto Mlalakuwa eneo la Mikocheni, ni moja ya majengo yaliyoamriwa kubomolewa na mamlaka juzi.
Meneja wa gereji ya Spring, Yu Xiangqian, ambaye ni raia wa nchini China, alikutwa na Nipashe jana akiamuru wafanyakazi wake waondoe magari ya wateja ndani ili kuyatafutia hifadhi sehemu nyingine.
“Tayari nimeshaambiwa niondoke tangu jana (juzi), na gereji yangu nimeipima tayari iko ndani ya mita 60 kutoka mtoni. Nalazimika kuanza kubomoa kabla wahusika hawajaja kunibomolea nisije kupata hasara,” alisema.
Alisema ana magari zaidi ya 100 ambayo atayatafutia hifadhi kwa marafiki zake kabla ya Jumanne ambayo ndiyo siku ya kuanza kwa bomoa bomoa.
Bomoabomoa kubwa ambayo mpaka sasa imeelezwa kuhusisha nyumba 1,400 zilizo katika mabonde ya Mto Msimbazi na Mto Mlalakuwa, inatekelezwa kwa pamoja baina ya Baraza la Mazingira (NEMC), Wizata ya Ardhi na Makazi na Hamashauri ya Jiji.
Tayari nyumba 300 zilizo katika bonde la Kinondoni Mkwajuni na Hananasif zilivunjwa katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo mwishoni mwa mwaka jana, kabla ya kusimamishwa kwa muda.
Meneja wa gereji ya Spring, Xiangqian alisema alipanga eneo hilo na kwamba hakupewa taarifa na mwenye jengo juu ya ubomoaji huo.
“Hii taarifa ya kubomoa tumechelewa kuipata hivyo tunalazimika kuhama haraka ili kuokoa magari ya watu waliyoyaleta kuyatengeneza," alisema.
Aidha, Xiangqian, alisema ana mpango wa kukutana na mamlaka husika kuomba kuongezewa siku, ili aweze kuondoa vifaa vyake na kuepuka hasara zinazoweza kutokea.
Wakati huo huo, Mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), imemtaka mmiliki wa Gereji ya Spring, kusafisha Mto Mlalakua baada ya kubaini utiririshaji kinyesi kwenye mto huo.
Mwanasheria wa NEMC, Heche Suguti alitoa agizo hilo juzi baada ya kubaini gereji hiyo iliunganisha mabomba sita yanayotoa kinyesi ndani na kutiririsha maji taka hayo Mto Mlalakua.
“Tumefika hapa kuwaeleza kuwa wanatakiwa wahame, lakini pia tumebaini huyu raia wa China alikuwa hajachimba karo la majitaka na badala yake ameunganisha mabomba sita yanayotiririsha uchafu kwenda mto huu," alisema Suguti.
Hata hivyo, Nipashe lilifika eneo la tukio jana na kubaini mmiliki huyo hajasafisha mto huo.
“Hatuwezi kusafisha mtaro wakati tunatakiwa kuhama kuanzia leo (jana), tulichofanya ni kuzoa takataka,” alisema Xiangqian.
Nipashe jana lilifika maeneo hayo na kushuhudia wakazi hao wakiendelea na shughuli ya kuhamisha vitu vyao kutoka ndani ya nyumba zao pamoja na kazi ya ubomoaji wa hiyari ukiendelea.
Aidha, Nipashe lilishuhudia wakazi wa mtaa wa Coca Cola ambao ni sehemu ya nyumba hizo 600 wakiendelea na kazi ya kuhamisha samani za ndani jana.
“Hatuna jambo lingine la kufanya, ni kuondoa vitu vyetu ili tuangalie maisha mengine,” alisema Maria Shayo.

Habari Kubwa