Bunge hili patachimbika

25Jan 2016
Sema Usikike
Bunge hili patachimbika
  • • Bomoabomoa Zanzibar kuzua balaa

VIKAO vya kwanza vya Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huenda vikawa na changamoto nyingi kuliko vingine vilivyowahi kufanyika, kufuatia nguvu ya upinzani kuongezeka bungeni sambamba na changamoto lukuki, imeelezwa.

Spika wa Bunge Job Ndugai

Kutokana na hali hiyo, Spika wa Bunge hilo Job Ndugai ametakiwa kutambua nguvu hiyo ya upinzani na kuwashirikisha kikamilifu kwenye hoja mbalimbali bila kuegemea chama chochote cha siasa, kinyume chake patachimbika.
Hii maana yake ni kwamba hatua yoyote ya ubaguzi ama upendeleo, itazua balaa kubwa kwa Spika huyo na uongozi mzima wa bunge, kuliko faida.
Bunge hili linaloanza vikao vyake Mjini Dodoma kesho, linakutana wakati nchi ikiwa imegubikwa na aibu kubwa kitaifa na kimataifa.
Aibu hiyo ni kutokana na kuvurugika kwa uchaguzi wa Zanzibar na baadaye mazungumzo ya kuleta ‘muafaka’ yaliyokuwa yanaendelea, nayo kuonekana kama yamekwama.
Itakumbukwa kwamba wakati wa ufunguzi wa bunge hili la 11 wapinzani walisusia ufunguzi huo kwa madai ya kutaka Maalim Seif Sharif Hamad aliyegombea kiti cha urais kwa tiketi ya CUF, huku akifunikwa na mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), aapishwe kuwa rais kwa vile alishinda.
Japokuwa walitolewa kwa nguvu bungeni kwa amri ya Spika, lakini mazingira yanaonyesha kwamba bado madai yao yapo palepale.
Huenda safari hii suala hilo likawa kama tindikali kwa vile pande zote mbili zinazosigana ni kama zinalumbana kwa vile kila mmoja anasema lake.
Imeelezwa kwamba jambo lililochangia utulivu wakati wote tangu uchaguzi huo ufanyike ni mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea, hivyo kukwama kwake huenda kukalitibua bunge.
Jambo jingine zito ni hatua ya bomoabomoa ya nyumba za wananchi wanaodaiwa kuishi mabondeni.
Hata hivyo wachunguzi wa mambo ya siasa wanasema hoja hii inatazamiwa kuwa kali zaidi kwa vile inahusu pande zote mbili yaani upinzani na CCM.
Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Profesa Mwesiga Baregu alipokuwa akizungumza na SEMA Usikike kufuatia upinzani kususia uteuzi wa Kamati za Bunge.
"Bunge hili linaweza kuwa na hoja nzito ikiwamo ya mgogoro wa Zanzibar na bomoabomoa, hivyo kuleta mvutano mkali sana kuliko vikao vingine vyovyote vilivyowahi kufanyika, hivyo ni lazima Spika awe makini asiegemee upande wowote," alisema Prof Baregu.
Msomi huyo alisema kuwa upinzani ukitengwa kwenye hoja mbalimbali ama kuburuzwa, kunaweza kutokea mambo ambayo hayakutarajiwa na Watanzania ikiwa ni pamoja na wabunge kususa.
Alisema kuwa Watanzania wanataka kuona mabadiliko ambayo yalikuwa yakinadiwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu yakianzia bungeni kwa wabunge kuisimamia na kuishauri serikali na sio kuitetea hata kwa mambo ambayo hayapo.
"Kwanza serikali yenyewe haijatulia, mawaziri hawajatulia, hawajui wataibukia wapi, ni vyema wakatulia ili wananchi wajue vipaumbele vyao ni vipi, wana dira gani, mwelekeo na malengo gani ili wachangie," alisema.
Alisema kuwa hoja kuhusu utendaji huo wa serikali zinaweza kujitokeza bungeni, hivyo ni vyema Spika akaziruhusu hasa kwa kuzingatia kwamba hata rais mwenye alishasema kuwa hataki mawaziri wawe na majibu yasiyoeleweka.
“Spika anatakiwa awe mtulivu, aongozwe na busara, haki na uzalendo. Vinginevyo akileta mambo ya chama kushika hatamu, bunge hataliweza,”alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alisema kuwa safari hii anatarajia kuwapo mnyukano mkali bungeni wenye lengo la kuleta mabadiliko ambao wananchi wanayataka.
Dk. Bana aliwataka wabunge wajielekeza kwenye mabadiliko kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi badala ya posho na kuwataka wabunge wajue kuwa ubunge sio sehemu ya kutafuta kipato bali ni kazi ya utumishi.
"Wajenge hoja zinazolenga kuleta mabadiliko ya kweli kwa ajili ya maendeleo, kwa sababu wao ndio watunga sheria, wakiegemea kwenye maslahi yao ama ya vyama vyao hawatakuwa wamewatendea haki Watanzania waliowachagua," alisema Dk. Bana.
Dk. Bana pia amewataka wabunge kuwa na lugha ya staha na kuheshimu kiti cha Spika kwa kufuata kanuni, kwa vile Bunge linaendeshwa kwa mujibu wa kanuni.
"Wingi wa wabunge wa CCM ama upinzani uwe na manufaa, wasiende kuonyeshana ufundi wa kuongea bali wa kujenga hoja zenye mashiko kwa Watanzania kwani bungeni ni mahali pa kutulia na kujenga hoja," alisema.
Alifafanua kuwa bungeni ni mahali pa kutulia kwa umakini ili pale mbunge anaposimama kuzungumza aonekane amejipanga vizuri kama ambavyo wamekuwa wakifanya baadhi ya wabunge.
Alisema kuwa wapo Bunge lijielekeze kwenye mabadiliko kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi badala ya posho kwa kuwa kazi ya ubunge sio kutafuta posho bali ni utumishi.
"Jambo lingine ni kwamba wabunge wawe na lugha ya staha na kuheshimu kiti cha Spika kwa kufuata kanuni, kwa sababu Bunge haliendeshi kienyeji bali kwa kanuni,"

Habari Kubwa