Barnaba: Ni heshima kuwa balozi 'Amua'

24Mar 2017
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Barnaba: Ni heshima kuwa balozi 'Amua'

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya Barnaba, amesema kwake ni heshima kuteuliwa kuwa balozi wa mradi wa 'Amua Accelerator' ambao ni maalumu kwa ajili ya kutoa elimu ya Afya ya uzazi kwa vijana.

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya Barnaba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Barnaba, alisema wapo wasanii wengi wakubwa nchini lakini kuteuliwa kwake ni heshima kubwa kwake na kwa familia yake.

“Kutokana na kuaminiwa huku, nitaitumia nafasi hii vilivyo katika kufikisha elimu iliyokusudiwa ambayo naamini itawasidia kuwaondoa vijana hapo walipo katika suala zima la mapambano ya athari zitokanazo na masuala ya uzazi,”alisema Barnaba.

Aidha, Barnaba alizitaja njia ambazo atazitumia kuelimisha vijana kuwa ni pamoja na kutumia mitandao yake ya kijamii ambayo inafuatiliwa na mashabiki wake wengi.

"Pia nitatumia nafasi kila nitakapopanda jukwaani kwenye maonyesho mbalimbali kutoa elimu hiyo kwa sababu vijana wengi hukusanyika kwa wakati mmoja kwenye maonyesho mbalimbali ya muziki," aliongezea kusema Barnaba.

Awali, Meneja wa mradi huo wa AMUA, Adam Mbyallu alisema wamemchagua msanii huyo kama njia rahisi ya kufikisha ujumbe kwa vijana kutokana na mvuto alionao kwa jamii hususani kundi la vijana.

Habari Kubwa