BEN POL: Siri ya kuimba ‘Tatu’ ni hizi….

10Jun 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
BEN POL: Siri ya kuimba ‘Tatu’ ni hizi….

WIMBO mpya wa Ben Pol, unaoitwa ‘Tatu’ umekuwa gumzo nchini na kusababisha baadhi wadau wa muziki kujitokeza kutoa maoni yao tofauti.

Ben PoL.

Katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii, watu mbalimbali wakiwamo wasanii, wamejitokeza kuuchambua kama umefanikiwa katika kuwakamata mashabiki wa muziki.

Wanamuziki kama Baraka The Prince na rapa Quick Rokka, wameongeza chachu baada ya kuibua mvutano mkali kuhusu ubora wa mapigo ya muziki huo.

Barakah kwa upande anadai wimbo huo ni mbaya, huku akichagiza kwamba mapigo ya wimbo huo haueleweki na upo tofauti na ulivyotangazwa kabla ya kutoka.

Rokka kwa upande wake amekosioa maoni hayo, akidai si haki kwa sababu Ben Pol ameonyesha njia mpya ya muziki, vyema akapongezwa na si kumkatisha tama.

Kutokana na malumbano hayo makali kutawala, BT ilimtafuta Ben Pol na kufanya naye mahojiano maalum kwa lengo la kufafanua maoni hayo.
BT: Siku za hivi karibuni kumeibuka majadala mkali kuhusu wimbo wako ‘Tatu’, wewe kama mwimbaji unajisikiaje?

Ben Pol: Ukifanya kitu na kuleta mjadala ndani ya jamii, unajisikia vizuri kwa sababu inakupa chachu kwenye kazi yako.

BT: Wakati watu wanajadili muziki wako kwa nini umejiweka pembeni, bila kufafanua kile wanachokiona kuna utata?

Ben Pol: Si lazima uwepo kwenye mazungumzo, lakini itafikia wakati utazungumza baada ya kusikia maoni ya watu, leo nafanya hivyo ingawa naweka tahadhari nisije nikaharibu mjadala huo.

BT: Mabishano yamejikita katika mapigo (Beat) za wimbo wako wa ‘Tatu’, baadhi ya wasanii wanadai ni mbaya na haulingani na hadhi yako. Je kuna ukweli?
Ben Pol: Nataka kukuambia jambo moja, nyimbo yangu imeleta ladha mpya ya muziki ambayo wengi hawajaielewa, lakini kuna wale waliotambua na kunielewa, wao wananipongeza?

BT: Je ulifahamu siku moja utafanya jambo ambalo lingeleta mgawanyiko?

Ben Pol: Nilipoingia studio niliona ni muziki wa kawaida tu ninaorekodi, nilifanya ubunifu wangu wa kuchanganya mapigo ngoma za asili ya Kihaya, lakini sikutarajia kama siku moja watu wataujadili kama ilivyo sasa.

BT: Kwani ubunifu wako wa muziki umeuita jina gani?

Ben Pol: Haha hahaha…Hapana, hata mimi siwezi kuita jina gani, lakini ndani yake kuna ladha ya makabila ya Kihaya, Kigogo na Wanyakyusa. Kama ukisikia vyema utagundua hilo. Lakini nawaachia mashabiki waseme hasa pale wakiona video yake wiki inayokuja.

BT: Tumemsikia wasanii wakitofautiana kwamba aina ya muziki wako ni mbaya na wengine wanasema upo sawa, Je kwanini hukufuata aina ya muziki uliouzoea na uliokufanya uwe maarufu?

Ben Pol: Msanii anayesema maneno kama hayo hana uwezo wa kufikiria na kutambua nini nimefanya ndani yake, kila mwenye ufahamu anajua ubunifu niliofanya. Siwezi kukatishwa tamaa na maoni ya watu kama mwenyewe nafahamu nipo sahihi.Wasanii wengi ni wavivu tunakwenda na trend.

BT: Je unadhani wasanii wa Bongo si wabunifu?

Ben Pol: Hapana sijasema hivyo, ila kuna tabia ya kufuata upepo, ukiibuka mtindo wa muziki wa kigeni wote tunakwenda huko. Anapotokea mtu akabuni kitu kipya wanajitokeza wasiopenda.

BT: Kabla hujaachia ngoma ya ‘Tatu’ jamii ilishtushwa na zile picha za kutangaza wimbo wako, Je unaona ulikuwa sahihi kufanya vile?

Ben Pol: Yaah, nilifanya kwa usahihi kulingana na kile nilichotaka kuelezea ndani ya wimbo wangu. Sina la kusikitika kwa kile nilichofanya kwa sababu naamini binadamu wana tabia ya kuzoea jambo na pale ukifanya tofauti watashtuka.

BT: Mashabiki na watu mbalimbali walimjua Ben Pol ni kijana mtulivu, mwenye maadili, asiyependa kashfa au kwenda kinyume na jamii wanavyotaka. Unadhani mabadiliko haya ya muda au yataendelea?

Ben Pol: Ni kweli watu walizoea kuniona katika hali ile, lakini kila siku mambo yanabadilika, lazima utasukumwa kama maji ya masika, watu wakubali kwamba Ben Pol hataweza kuishi maisha yale yale bila kubadilika. Nawaomba wanielewe kwamba wataendelea kuona mabadiliko mengi kwani ndiyo maisha yalivyo.

BT: Unaweza kueleza ulipoweka picha ya kwanza nani alikuwa wakwanza kushtuka?

Ben Pol: Dah, alikuwa mpenzi wangu ambaye alipoona tu, alishtuka na kuniamba kitu gani hiki? Lakini nilijaribu kukaa naye chini na kumwambia madhumuni ya kufanya vile. Nashukuru Mungu alinielewa na kunishika mkono.

Habari Kubwa