Diamond, Ali Kiba kuipigia debe Serengeti Boys

01Mar 2017
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Diamond, Ali Kiba kuipigia debe Serengeti Boys

WASANII nyota wa muziki wa kizazi kipya wa hapa nchini, Abdul Naseeb 'Diamond Platinumz' na Ali Kiba,

Jana walitangazwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Uhamasishaji ya timu ya soka ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), ambayo inajiandaa kushiriki fainali za Afrika zitakazofanyika Aprili mwaka huu.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, aliitangaza kamati hiyo jana wakati akizungumza na wadau wa michezo kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Waziri Nape alisema lengo la kuiteua kamati hiyo ni kutaka kukusanya fedha na kuhamasisha Watanzania kuisaidia timu hiyo pamoja na maandalizi ya kuandaa michuano ya vijana ya Afrika itakayofanyika nchini mwaka 2019.

Waziri huyo alimtaja mwenyekiti wa kamati hiyo kuwa ni Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Azam, Charles Hillary, katibu wao ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa.

Wajumbe wengine ni pamoja na Eric Shigongo, Ruge Mutahaba, Beatrice Singano, Hoyce Temu (Miss Tanzania 1999), Maulid Kitenge na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Hassan Abbas.

Serengeti Boys imepangwa katika Kundi B lenye timu za Mali, Angola na Niger wakati Kundi A linaundwa na wenyeji Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana.

Fainali hizo zitafanyika kuanzia Aprili 21 na timu nne zitakazofanya vizuri zitakata tiketi ya kushiriki kwenye mashindano ya Kombe la Dunia ya Vijana yatakayofanyika India baadaye mwaka huu.

Habari Kubwa