Diamond, Nandy na Harmonize vinara kusikilizwa 2019

28Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Diamond, Nandy na Harmonize vinara kusikilizwa 2019

JUKWAA namba moja kwa huduma ya kupakua muziki barani Afrika, Boomplay imemtaja msanii Diamond Platnumz, kuwa ndio mwanamuziki aliyesikilizwa zaidi Tanzania, kulingana na taarifa rasmi za muziki mwaka 2019.

Taarifa hiyo iliyowekwa kwenye ripoti maalumu kuhusu muziki imeegemea zaidi takwimu kutoka kwenye jukwaa hilo ambalo lina watumia zaidi ya milioni 60, ulimwenguni kote huku Tanzania kukiwa na watumiaji zaidi ya milioni 4.2. 

Boomplay inajivunia kuwa na aina tofauti za nyimbo ambazo idadi yake ni zaidi ya milioni 20, ambazo zinapatikana kwenye iOS, Android na web.

Nafasi ya pili imenyakuliwa na mwanadada Nandy, na ya tatu imechukuliwa na Harmonize huku Rayvanny akishika namba nne. Msanii wa zamani wa kundi la Yamoto, Aslay amekamata namba tano, huku namba sita ikinyakuliwa na Mbosso, Jux  nafasi ya saba huku Lava Lava akishika namba nane, mwanamuziki pekee wa injili katika orodha hii ni Joel Lwaga aliyeshika namba tisa na namba 10 akisimama mwanadada shupavu Vanessa Mdee.

Mbali na wasanii, Boomplay pia imekusanya taarifa kuhusu nyimbo ambazo zimesikilizwa zaidi pamoja na albamu, ambapo wimbo wa Diamond Platnumz akiwa na Fally Ipupa ‘Inama’ ndio umetisha zaidi kwa mwaka 2019. Albamu ya Nandy ya “The African Princess” imeshika namba moja, huku “The Love Album” ya Jux ikishika namba mbili na kufuatiwa na “A Boy From Tandale” ya Diamond Platnumz iliyoangukia namba tatu.

Boomplay pia imetoa taarifa za mwenendo na tabia za namna muziki unavyosikilizwa Tanzania. Katika taarifa hiyo maalumu, Nyimbo Za Injili (Gospel) zimeonekana kusikilizwa zaidi na kufuatiwa na miondoko ya Bongo Flava, kisha Afrobeats inashika namba tatu, huku ya nne na tano zikishikwa na Hip Hop & Rap pamoja na Reggae.

Habari Kubwa