GABO, WEMA wageuka ‘Kisogo’ filamu za bongo

17Jun 2017
Adam Fungamwango
Dar es salaam
Nipashe
GABO, WEMA wageuka ‘Kisogo’ filamu za bongo

WATU wamelalamika sana. Wameilalamikia tasnia ya filamu nchini juu ya kushuka kwa viwango.

Wengi wanadai hazita tena ubora, tunzi zao zinaboa na zinafanana kinachotofautisha ni mtiririko tu. Pia wasanii wenyewe ama wamejisahau au wamelewa na sifa za ustaa.

Wanaoingia kwenye tasnia hiyo wengi wao hawana ujuzi, kitendo ambacho kimechagia soko la filamu bongo movie kuanguka.

Kila msanii analalamika.

Cha ajabu ni kwamba kila mtu analalamika. Msanii analalamika kukosa soko na kukimbilia kuzituhumu mamlaka za nchi kuingiza filamu kutoka nje ya nchi ambazo zinasababisha zao zidode sokoni. Wengine wakaandamana.

Hata hivyo wachunguzi wa mambo wakajiuliza, filamu za nje zipo tangu hata wasanii wa Tanzania hawajaanza kuigiza. Na hata walipoanza kuigiza na kupata umaarufu mkubwa na soko kuwa zuri, bado filamu za nje zilikuwapo.

Kikubwa kinachosababisha soko kushuka ni ubora tu. Wanunuzi nao wanalalamika na kuona kama wanaibiwa. Na hii ndiyo imesababisha kususa kufanya filamu zisinunulike dukani. Lakini wakati wasanii wengi wakikalamika, msanii Salim Ahmed maarufu kama 'Gabo Zigamba' yeye alikaa chini na kutafakari.

Akajiuliza nini kimetokea? Tatizo liko wapi? Alipojua akaamua kuja na suluhisho.

Ameibuka na filamu mpya iitwayo 'Kisogo'. Mwenyewe anaamini kuwa ni filamu inayoleta mkombozi na italeta mapinduzi makubwa kwa kipindi hiki ambacho soko limepungua mno.

Anaanzia kwenye utunzi wa filamu yenyewe. Ina kisa ambacho si rahisi sana kukiona kwenye filamu nyingi. Gabo amecheza na mmoja wa wasanii maarufu nchini, Wema Sepetu.

Ni wazazi wanaotumia muda mwingi kwenye kazi zao, bila kuwa karibu na mtoto. 'Hausigeli', ndiye anayeachiwa jukumu hilo kwa asilimia zaidi ya 90.

Hata hivyo mfanyakazi huyo si mtu mzuri. Ni mchawi. Mtoto anaumwa, wazazi hawajui nini kinaendelea. Kumbe anayemlea ndiye anayemtesa mtoto.

Hapo ndipo utamu wa filamu hiyo unapokolea, wazazi, ndugu na jamaaa wakihangaika huku na huko, kutafula 'kinachomla' mtoto.

Ni funzo kwa wazazi hasa wa mijini ambao hawana tabia au muda wa kukaa na watoto zao na kuwaachia wafanyakazi wa ndani kwa kisingizio wanachokiiza 'wapo bize'.

Mapinduzi mengine ya filamu hii kuwa ni fupi ya dakika 30 pekee. Itakuwa ni mara ya kwanza kwa filamu ya Kibongo kuwa na dakika chache kiasi hiki. Pamoja na kuwa ina dakika hizo, lakini kila kitu kimekamilika na kuachana na kuonyeshwa kwa vitu vingi ambavyo havina maana.

Nimeangalia picha nyingi chini. Nyingi zina sehemu ya kwanza na ya pili. Lakini ukiziangalia kwa makini na jicho la tatu zilitakiwa ziwe chini ya dakika 30 au 45 tu na na si saa moja na nusu au masaa mawili kwa sehemu ya kwanza na ya pili.

Gabo anakiri kwamba hakuna filamu iliyotokana na wazo la kipekee Duniani, ila baadhi ya wasanii hawajui kuweka uhalisia kwa kuwaaminisha watazamaji kwamba yule anayemuona ni afisa serikalini, mgambo, masikini au tajiri.

Pia watu wamechoshwa kudanganywa kulazimishwa mchana kuwa usiku, au mtu mwenye akili timamu kuitwa mwenye matatizo ya akili.

“Tunataka kuondoka huko, kupitia Kisogo tumeweka uhalisia wake ili kila mtu anayeangalia aweze kuamini na kufurahi,” anasema Gamba.

Maneno ya Gamba ni uthibitisho kwamba wasanii na watengenezaji filamu wamekuwa wakiongeza vitu vingi ambavyo havihitajiki na havina muunganiko wowote kwa lengo tu ya kuifanya kuwa ndefu.

Wakati mwingine uanweza kuona mhusika anatoka dukani na kulifuata gari lake. Hapo inaweza kutumia dakika hata tano anatembea tu, kitu ambacho ni kupoteza muda tu.

Kingine ambacho Gabo amejiongeza ni kutotegemea mauzo ya filamu hiyo kwa nakala za DVD tu peke yake, badala yake amekwenda mbali zaidi.

Kutokana na teknolojia kukua duniani kwa sasa, ameamua pia kuiweka kwenye kitu kinachoitwa 'Mobile App'. Hii inamfanya yoyote aliye na simu ya mkononi ua kufuta kuweza kuiona akiwa sehemu yoyote ile, iwe mjini, kijijini au shambani na si kusubiri mtu hadi siku apate nafasi aende mjini ndipo atafute nakala ya filamu.

Huu ni mwanzo mzuri wa mapinduzi ya filamu. Gabo ameanza na waliobaki wafanye hivyo. Wabuni mbinu mbalimbali zitakazowafurahisha na kuwarudisha tena wateja wa filamu nchin. Wakichanga na hizi za Gabo, nadhani mambo yatarejea kama zamani na watafaidika na matunda ya jasho lao.

Habari Kubwa