Inakuawaje usimulie undani wa mpenzi wako?

02Jul 2017
Mary Geofrey
Dar es salaam
Nipashe Jumapili
Inakuawaje usimulie undani wa mpenzi wako?

NI jambo linaloleta fahadha na mshtuko pale unaposikia mambo yako ya ndani yamezagaa hadharani, tena unakutana na watu wanaanza kukuchambua na kuonekana si lolote.

Unapofuatilia kiini cha kuzagaa kwa taarifa hizo, unagundua mwenza wako ndiyo chanzo, yeye ndiye kayasimulia mambo yenu ya faragha.

Matukio kama haya yanatokea katika jamii, utakuta mtu ambaye anajiheshimu lakini mambo yake yote yapo wazi, kila anapopita anaonekana si kitu.

Hayo yote yanatokana na mtu mmoja tu, ni mpenzi wake wa kike au kiume kuwa na tabia ya kusimulia kila kinachofanyika ndani ya nyumba.
Naweza kusema tabia hii ni mbaya, sawa na sumu inayoweza kummaliza mtu taratibu bila mwenyewe kujua.

Unaweza kudhani kuwa hakuna mtu wa aina hii, lakini nikuhakikishie tu wapo na na wanaishi ndani ya jamii zetu. Hawa hawana vifua vya kuhifadhi kitu, midomo yao ipo wazi, wao husema chochote kwa kutaka sifa au kumdhalilisha mwenzi wake.

Unakutana na mwanamke au mwanaume ambaye ana akili zake tu timamu amekaa sehemu na wenzake anaanza kusimulia namna anavyoishi na mwenza wake, mengine ya ndani kabisa.

Wanaozungumza mambo ya wenza wao si tu wale walioachana tu, bali wapo hata wale ambao wanadumu kwenye uhusiano.

Unakuta dume zima amesimama na kuwaeleza marafiki zake namna anavyoishi na mpenzi wake, huku wenzake wakimpokea kwa kicheko.

Mbaya zaidi anaeleza mapungufu yote ya mwenza wake, ikiwamo vitu vinavyomfurahisha na kumchukiza kwenye mapenzi yao.

Mwanamke naye utamsikia amekaa na wenzake anaelezea mapungufu na kasoro za mwanamume wake, bila kufikiria hao anaowaeleza wanamanufaa gani au watamsaidia nini.

Kibaya zaidi watu kama hawa huelezea mabaya au mazuri ya wenza wao, lakini wana tabia ya kujikinga na kujilinda dhidi ya mambo yake binafsi.

Jambo la kujiuliza kama wewe ni mwanamke ulimkubalia mwanaume kwa moyo wako wote, ulitarajia nini pale ulipokubali kuanzisha Uhusiano? Kama matarajio yako hayakufikiwa, kutangaza mambo yenu ya siri ndiyo utapata suluhisho?

Majibu ya maswali hayo ni kwamba watu wa aina hiyo, huwa hawajiamini na kutawaliwa na ushamba wa mapenzi.

Ni ulimbukeni wa hali ya juu kutoa mambo ya ndani kwani humtoa akili yule anayesimulia na kumdhalilisha muhusika bila sababu ya msingi.

Ni vyema kila mmoja kujizuia kuwa msemaji wa uhusiano wenu. Kama kuna kasoro au kupongezana lazima mzungumze peke yenu, wala msiwashirikishe watu.
Mwanamke au mwanaume ambaye ana tabia ya kusimulia mambo ya ndani, utangundua kuna tatizo la kimaadili wakati wa ukuaji wake.

Huwezi kukutana na kijana au binti ambaye anamaadili aliyefunzwa na wazazi wake anafanya mambo kama hayo ya kutangaza mambo ya mwenza wake kwa watu wengine.

Habari Kubwa