Jay Dee atambulisha 'Anaweza'

23Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jay Dee atambulisha 'Anaweza'

MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Judith Wambura, maarufu "Lady Jay Dee" ameendelea kuonyesha ukongwe wake katika sanaa hiyo baada ya jana kutambulisha kibao chake kipya kiitwacho Anaweza.

Lady Jay Dee

Lady Jay Dee au Komando ameutambulisha wimbo huo sambamba na kutoa video ili kuwavuta karibu mashabiki wake ambao wanafahamu kiwango chake.

Akizungumza na gazeti hili jana, Lady Jay Dee, alisema kuwa kibao hicho amekitengenezwa na mtayarishaji Spicy Judoka wa Nigeria huku video ikisimamiwa na Justin Compus Lutona wa Afrika ya Kusini na lengo la kuchanganya wataalamu hao ni kuhakikisha kazi yake inakuwa na hadhi ya kimataifa.

Alisema kuwa baada ya kukamilisha kazi hiyo, anajiandaa kufanya onyesho la muziki na tayari ameanza maandalizi kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wake.

Aliwataja wasanii wengine ambao wanamuunga mkono kuwa ni Rutta Bushoke, Nikki Mbishi na Judoka anayeimba muziki wa Hip Hop na kueleza kuwa nyota wengine atawatangaza hapo baadaye.

“'Nimemiss' jukwaa, nimemiss watu wangu, nimemiss ile kazi ya kusimama masaa kadhaa na kuwasiliana na watu wanaounga mkono muziki wangu kwa miaka nenda, rudi.

Nimeamua sasa kuwa nitafanya haya matamasha mara kwa mara ili mwisho wa siku muziki wangu uendelee kuishi miongoni mwa mashabiki wangu kwa sababu tukisema ukweli ndio kitu ninachokipenda, muziki”, alisema Lady Jay Dee ambaye ana albamu saba.

Habari Kubwa