Jimmy Master kuleta mapinduzi ya filamu

04Jul 2016
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Jimmy Master kuleta mapinduzi ya filamu

KWA wale wanaofuatilia burudani za filamu nchini, Jimmy Mponda maarufu 'Jimmy Master' si jina geni kwao kutokana na msanii huyu kutayarisha filamu za mapigano zilizomfanya awe na jina kubwa.

Jimmy Mponda maarufu 'Jimmy Master'

Msanii huyu ni mmiliki Kundi la Sanaa la Mzimuni ambaye sasa anakuja na filamu mpya aliyoipa 'The Foundation', ambayo ina matukio ya kimapigano.

Maandalizi ya filamu hiyo sasa yako katika hatua za mwisho na wakati wowote itaingia sokoni.

Jimmy Master ni mmoja wa waanzishili wa filamu za mapigano nchini aliyewahi kutamba na filamu mbalimbali baadhi zikiwa ni 'Shamba Kubwa', 'Unga Adui', 'Kifo Haramu', 'Usia', 'Misukosuko' na 'Double '.

"Nimekuja na filamu kali ya 'action' ambayo imerekodiwa kisasa, wasanii wote walioshiriki wamefanya vizuri katika nafasi zao, hivyo mashabiki wajiandae kupata uhondo wa nguvu na mafundisho kuhusu matukio ya kila siku katika jamii," alisema Jimmy na kuongeza:

"Ili kufanikisha kazi hii, umakini unahitajika kwa kiasi kikubwa, kwenye tasnia yetu ya filamu siku zote mashabiki wetu wanahitaji kuona 'muvi' ikiwa na uhalisia siyo porojo, hakuna kitu kigumu kama kumfanya mtu akuamini na kukubali kazi yako."

Alisema kuwa 'The Foundation' ambayo anatarajia kuitambulisha hivi karibuni, itarudisha heshima ya filamu za mapigano nchini na kuwafanya mashabiki waendelee kupata burudani kama ilivyokwa miaka ya nyuma.

Nyota huyo alisema kuwa filamu ya ‘Misukosuko’ ilikuwa gumzo kwa kupata mashabiki wengi na kuifanya iwe na sehemu tatu kwa ajili ya kukidhi kiu ya mashabiki wake.

"Safari hii ninataka The Foundation iwe zaidi ya Misukosuko kwa sababu nilikuwa kimya kwa muda mrefu nikijipanga vizuri, hivyo nina uhakika itafanya vizuri kuliko filamu zangu zilizotangulia," Jimmy Master aliongeza.

ALIVYOJITOSA KATIKA SANAA
Anasema alianza sanaa kwa kujihusisha na mchezo wa sarakasi mwaka 1978 hadi 1980 alipojiunga na Kikundi cha Yusta ambacho kilijihusisha na sarakasi, ngoma na maigizo ya jukwaani.

Ilipofika mwaka 1986 alihamia Arusha kwa ajili ya kujishughulisha na biashara na akiwa huko aliendelea kushiriki sanaa kwa kufanya mazoezi kwenye Kituo cha YMCA.

"Nikiwa katika pilika pilika za kibiashara nilikutana na wenzangu na kuanzisha Kundi liitwalo Black Ninja, tulikuwa tukiandaa shoo za mapigano," alieleza.

Anasema kuwa walianza kupenyeza sanaa yao hiyo kwa kuvuka mipaka ya nchi kwa kufanya ziara Kenya na Uganda kati ya mwaka 1992 hadi 1993 na filamu yake ya kwanza kuandaa ilikuwa ni 1994.

"Tulitafuta mtunzi wa kuchukua matukio ya video na kuandaa fialmu ya ‘Shamba Kubwa’ baada ya kukamilika filamu hiyo tuliizindua huko Tanga na kuanzia hapo nilibakiza asilimia 60 katika filamu na asilimia 40 kwenye mawazo ya biashara," aliongeza Jimmy Master.

Msanii huyo alitambulisha sokono filamu ya pili iitwayo 'Unga Adui' mwaka 1996 ikiwa ni ya mapigano, ambayo nayo ilitangaza vyema jina lake.

"Mwaka 2005 nilitoa filamu ya 'Misukosuko' ambayo ilidumu sokoni hadi mwaka 2010 na kisha mwaka 2012 ikaja nyingine ya Double J' ambayo ninaweza kusema ilikuwa ya mwisho kwani tangu kipindi hicho nilikuwa sijaandaa filamu nyingine."

Jimmy Master aliongeza kuwa baada ya kimya cha miaka mitatu sasa kupitia Mzimuni Theatre Arts’ amevunja ukimya 2016 kwa kuja na filamu mpya.

Aliwataja wasanii walioshiriki kwenye filamu hiyo mpya ni yeye mwenyewe , pacha wake Sebastian Mwanangulo 'Inspector Seba', Christina Aidan, Said Ndomboroa, Mariamu Mustafa, OP Mohamed 'Guga' na Ramadhan Mohamed 'Junior'.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa