Kifo cha msanii wa The Mafik chazua maswali

16Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kifo cha msanii wa The Mafik chazua maswali

Msanii kutoka kundi la The Mafik, Abdallah Matimbwa maarufu Mbalamwezi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo kutokana na majeraha ambayo yanahisiwa kuwa amepigwa na watu wasiojulikana na mwili wake kuokotwa ukiwa hauna nguo.

Abdallah Matimbwa maarufu Mbalamwezi.

Akizungumza na The Guardian Digital, leo mmoja wa wasanii wanaunda kundi hilo Hamadai amesema taarifa za kifo Mbalamwezi alizipata jana jioni, ambapo kabla ya taarifa hizo tayari walikuwa wakimtafuta kwa siku tatu bila mafanikio.

"Taarifa za kifo chake (Mbalamwezi) nilizipata jana jioni, kabla ya kifo chake hakuonekana kwa siku tatu, hapa nilipo siwezi nikatoa taarifa zilizonyooka kwa sababu kifo chake kinahitaji maelezo nipo katika utaratibu wa kupata mwili wa ndugu yangu,"- amesema Hamadai.

Naye mjomba wa marehemu Chief Mponda, amesema taaraifa za kifo cha Mbalamwezi wamezipata saa 8 usiku wa kumakia leo Agosti 16, 2019 ambapo mara ya mwisho alizungumza na marehemu wiki moja iliyopita na kwa jinsi walivyokuwa wakizungumza alikuwa ni mzima wa afya.

Ameongeza kuwa chanzo cha kifo cha ndugu yake bado ajazipata vizuri kwani anawasubiri walienda Hospitali ya Muhimbili kufautilia na kuutambua mwili ili kufahamu zaidi.

Aidha mmoja wa meneja wanaolisimamia kundi la The Mafik amesema yupo njiani akielekea hospitali kuthibitisha ila taarifa hizo ni za ukweli na sababu ya kifo chake hakijatokana na ajali wala kuumwa kwakuwa hakuwa anasumbuliwa na ugonjwa wowote.

Aidha utata umegubika kifo chake ambapo marafiki zake wameeleza kuwa walikuta mwili wa  marehemu ukiwa umetelekezwa bila nguo  na kuupeleka katika hospitali ya Muhimbili.

Imeandikwa na Juster Prudence, TUDARCO