Kilichomuua Masogange

22Apr 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Kilichomuua Masogange

WAKATI mwili wa marehemu Agnes Gerald 'Masogange' ukitarajiwa kuzikwa mkoani Mbeya yalipo makazi ya familia yao, ugonjwa uliomsababishia msanii huyo kufikikwa na umauti umeelezwa.

Agnes Gerald 'Masogange'

Dada wa marehemu, Emma Gerald, aliliambia gazeti hili jana kuwa, kwa sasa wapo kwenye taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu huyo ambaye alikuwa msanii maarufu aliyetumika kupamba nyimbo za wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva.

Awali, kiongozi wa wasanii, Steve Nyerere, alisema kuwa wasanii kwa umoja wao wanashirikiana na familia kuusafirisha mwili wa marehemu Masogange kuelekea Mbeya.

"Tunatarajia kuzika Mbeya, kwa sasa tunaendelea na taratibu kwa kushirikiana na familia yake hasa ndugu waliopo hapa Dar es Salaam kuhakikisha tunausafirisha mwili wa mpendwa wetu," alisema Nyerere.

Alisema mara baada ya kikao wanafamilia watatoa taarifa ni lini mwili wa marehemu masogange utapumzishwa.

Kabla ya kifo chake,  imeelezwa Masogange alilazwa katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar es Salaam, kwa siku nne akisumbuliwa na ugonjwa wa pumu na tatizo la upungufu wa damu.

Masogange alianza kupata umaarufu baada ya kushirikishwa kama 'Video Queen' kwenye nyimbo ya msanii aliyekuwa akija juu kipindi hicho, Belle 9, wa 'Masogange'.

Wimbo huo ndio uliompachika jina la utani la Masogange ambalo limekuwa maarufu zaidi.