Kolabo Coke Studio 2017 yasukwa

31Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kolabo Coke Studio 2017 yasukwa

MTAYARISHAJI wa muziki na mwanamuziki nguli  nchini, Emmanuel Mkono maarufu kwa jina la Nahreel, akishirikiana na magwiji wengine wa kutengeneza muziki barani Afrika anaendelea kusuka 'kolabo' za wanamuziki ....

wanaoshiriki onyesho la Coke Studio linalotarajiwa kuanza kuonyeshwa kwenye vituo vya luninga mapema Septemba mwaka huu.

Nahreel ambaye ameandaa nyimbo nyingi bora za wasanii mbalimbali nchini zinazotamba katika soko la muziki ndani na nje ya nchi, pia ni mmoja wa wanamuziki wa Kundi machachari la Nevy Kenzo.

Akizungumza kuhusu onyesho hilo jana akiwa  Nairobi nchini Kenya, Nahreel alisema misimu minne ya Coke Studio Africa imekuwa na mafanikio makubwa katika kuutangaza muziki wa Bongo Flava barani Afrika. 

"Washiriki wamejiongezea mashabiki, wamejifunza mambo mengi kuhusu muziki kama burudani, muziki kama taaluma na muziki kama biashara na tena si tu kutoka kwa wasanii wenzao wa Afrika, bali wa Marekani pia," alisema.

Baadhi ya wakali wa kutengeneza muziki anaoshirikiana nao msimu huu ni  Yuvir Pillay Nivedan a.k.a Sketchy Bongo kutoka Afrika ya Kusini na Kiff No beat kutoka nchini Ivory Coast.

Kwa upande wa Ma-DJ wapo Tafinha kutoka Angola, Laura Beg (Mauritius), Jah Prayzah  na Slapdee (Jamhuri ya Afrika ya Kati), Bisa Kdei  na Worlasi (Ghana), Betty G (Ethiopia), Bruce Melodie, Shellsy Baronet  na Mr. Bow (Msumbiji), Denise (Madagascar) na Freeda kutoka Namibia.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Coca-Cola msimu wa Coke Studio mwaka huu utakuwa umesheheni burudani za muziki motomoto wenye vionjo vya Kiafrika kutokana na kuwaweka wasanii pamoja kutoka nchi 16 za  Afrika na kushirikiana kufanya kolabo ambapo onyesho lake   litaonyeshwa kwenye vituo vya luninga zaidi ya  nchi 30 barani Afrika.

Wasanii wanaoshiriki Coke Studio msimu huu wanatokea katika nchi za   Africa ya Kusini, Rwanda, Angola, Zimbabwe, Togo, Madagascar, Mauritius, Kenya, Uganda, Tanzania, Nigeria, Ghana, Msumbiji, DRC, Ethiopia na Cameroon.

Habari Kubwa