Lady Jay Dee afunguka Z'bar

21Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Lady Jay Dee afunguka Z'bar

MSANII mkongwe wa muziki wa bongo flava, Judith Wambura (Lady Jay Dee) ameitaka Serikali ya Zanzibar kuwashirikisha zaidi wasanii wa muziki ili kusaidia kuharakisha maendeleo katika sekta ya utalii visiwani humo.

MSANII mkongwe wa muziki wa bongo flava, Judith Wambura (Lady Jay Dee)

Lady Jay Dee alisema hayo juzi kabla ya kutumbuiza katika sherehe ya kuwapongeza wageni kutoka nchi zaidi ya 150 duniani ambao walishiriki katika Tamasha la Utalii Zanzibar mwaka huu.

Msanii huyo alisema wasanii watakaposhirikishwa watasaidia kuwavuta watalii kuongezeka kutokana na kazi wanazofanya kufahamisha katika mataifa mbalimbali.

Aliwashuruku waandaaji wa tamasha hilo kwa kumpa mwaliko wa kutumbuiza katika sherehe hiyo na kuahidi ataendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha malengo ya tamasha hilo yanafanikiwa.

"Ninayo furaha kubwa sana kuwa sehemu ya tukio hili leo (juzi usiku), linalohusu mafanikio ya Utalii wa Zanzibar," alisema Lad Jay Dee ambaye aliongeza kuwa yuko katika hatua za mwisho za kutambulisha kibao kipya ambacho anaamini kitaliteka soko la muziki huo wa kizazi kipya.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watembeza Watalii Zanzibar (ZATO), Hassan Ali Mzee, aliipongeza serikali kwa kuanzisha tamasha hilo ambalo linasaidia kuutangaza utalii na kisiwa hicho duniani.

Mzee alisema kuwa amani na utulivu uliopo visiwani hapa kwa sasa pia unawavutia wawekezaji na watalii ambao wanasaidia kuinua uchumi wa Zanzibar.

Naye Mkurugenzi wa mgahawa maarufu unaopendwa na watalii visiwani hapa uitwao 6 Degree South, Saleh Said, alisema kitu kinachowapa sifa ni huduma bora inayotolewa na wafanyakazi wake ambao ni raia wa Tanzania.