Lundenga aitema Miss Tanzania 

01Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Lundenga aitema Miss Tanzania 

HATIMAYE Kampuni ya Lino International Agency iliyoko chini ya Mkurugenzi wake, Hashim Lundenga "Uncle" imetangaza rasmi kuachana na mashindano ya urembo ya Miss Tanzania.

Akitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam, mbele ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Mngereza, Lundenga alisema kampuni yake ambayo iliandaa mashindano hayo kwa muda wa miaka 23, imefikia uamuzi huyo kwa "roho safi" huku ikijivunia mafanikio licha ya kukutana na changamoto mbalimbali.

Lundenga alisema kuwa kwa sasa jukumu la kuendesha mashindano hayo litakuwa chini ya kampuni nyingine iitwao The Look ambayo iko chini ya mrembo wa Taifa mwaka 1998, Basila Mwanukuzi.

"Tumeamua kuachia mashindano haya kwa roho safi, tumepitia katika faraja na changamoto nyingi kwa kuanzisha na kuandaa mashindano haya ambayo warembo wengi wamefanikiwa kubadili maisha yao kwa kupata mafanikio kupitia mashindano haya," alisema Lundenga.

“Tumeamua kuachana na mashindano haya bila ya kushawishiwa na mtu wala taasisi yoyote, tumefanya hivyo kwa nia njema kabisa, tunajivunia kuipaisha Tanzania mwaka 2005 kupitia Nancy Sumari ambaye alikuwa miongoni mwa nchi 10 bora duniani katika mashindano ya dunia, ni mafanikio makubwa zaidi katika sekta ya urembo, tulikuwa wa saba kati ya nchi zaidi 100 zilizoshiriki katika Miss World,” alisema Lundenga.

Kwa upande wake, Basila Mwanukuzi alisema kuwa  wamefarijika kupewa nafasi hiyo ambayo ni kubwa sana na kuomba msaada kutoka kwa wadau mbalimbali huku akieleza kuwa anazijua changamoto za mashindano hayo, kwa sababu yeye ni mmoja wa warembo walioshiriki akitokea katika Kanda ya Kinondoni hadi alipotwaa taji la Taifa.

 

Habari Kubwa