Miaka 20 ya Twanga kutingisha Oktoba 27

17Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Miaka 20 ya Twanga kutingisha Oktoba 27

HATIMAYE Tamasha la maadhimisho ya miaka 20 ya Bendi ya African Stars (Twanga Pepeta) sasa yatafanyika Oktoba 27 kwenye Ukumbi wa Life Park (zamani New World Cinema) uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta Luizer Mbutu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam

Tamasha hilo litapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii ambao wanafanya kazi pamoja na Twanga Pepeta katika kuendeleza sanaa nchini.

Kiongozi wa bendi hiyo, Luizer Mbutu alisema wamejiandaa vema na siku hiyo kutakuwa na ‘saprizi’ nyingi kutoka kwa wanamuziki wao na tamasha kwa ujumla.

Luizer alisema mbali ya nyimbo mpya, kutakuwa na staili mbalimbali za kunogesha onyesho hilo na kwamba zitakuwa zikionyeshwa kwa mara ya kwanza jukwaani.

Kiongozi wa shoo wa bendi hiyo, Super Nyamwela, alisema itakuwa ya tofauti ambapo watatambulisha madansa na waimbaji wapya wa bendi.

Miongoni mwao ni dansa Stella Manyanya. "Tuna 'crew' ya watu 18 ambao wamesheheni kila idara, kifupi siku hiyo Twanga mpya itaonekana," alisema Super Nyamwela.

Aidha, viingilio siku hiyo vitakuwa ni Sh. 10,000 kwa viti vya kawaida, 25,000 kwa VIP na Sh 250,000 kwa meza ya watu 10.