Mobeto, Uwoya waonywa TCRA

20Jul 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mobeto, Uwoya waonywa TCRA

WASANII nyota nchini Hamisa Mobeto na Irene Uwoya, wamepewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi kupitia kurasa zao za 'Instagram' kwa kosa la kutuma picha za utupu.

WASANII nyota nchini Hamisa Mobeto na Irene Uwoya.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitangaza maamuzi hayo jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuwahoji na kujiridhisha kutenda kosa hilo kinyume cha sheria za nchi na kanuni za maadili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Valeria Msoka, akitangaza maamuzi hayo pia aliwataka wasanii hao kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kutokutuma picha zisizo na maadili.

Akisoma kosa la msanii na mwanamitindo Mobeto, alisema alilitenda kosa hilo Juni 23 mwaka huu, kwa kutuma picha isiyo na maadili kupitia ukurasa wake wa 'Instagram' ikionyesha mama mjamzito akiwa ameshikilia tumbo juu kidogo ya sehemu zake za siri.

Alisema baada ya kumuita na kumuhoji Mobeto alikana kuhusika kuzituma yeye na kudai kuwa alizipiga mwaka jana akiwa mjamzito na kwa lengo la kutekeleza majukumu yake kama mwanamitindo.

Msoka alisema, kamati hiyo inamtuhumu kuhusika kupiga picha hizo za utupu ambazo zinaweza kuigwa na watoto na hazina maadili kwa jamii kinyume cha kanuni za maadili kifungu cha 5(a)(b).

Akimzungumzia Uwoya, alisema alikiri kosa la kupiga picha za utupu na kuomba radhi hali ambayo iliishawishi kamati kumpa onyo na kumtaka kuomba radhi.

Kwa upande wake, Uwoya aliwaomba radhi wasanii wenzake na kuahidi kuwa balozi wa kuhamasisha jamii kutokutuma picha zisizo na maadili.

Pia aliitaka TCRA kuanzisha semina elekezi ya wasanii ili kuwapa mafunzo namna ya kuepuka kutumia mitandao kinyume na kanuni za maadili.

Kwa upande wake Mabeto, aliahidi kuwa balozi mzuri wa kuhamasisha jamii kutokutuma picha zisizo na maadili.

 

Habari Kubwa