Msaga Sumu, Shilole jukwaa moja kesho

05May 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe
Msaga Sumu, Shilole jukwaa moja kesho

WASANII mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya na Singeli wa hapa nchini wanatarajia kutoa burudani katika onyesho maalumu litakalofanyika kesho kwenye Ukumbi wa JM uliopo Manzese jijini Dar es Salaam imeelezwa.

Shilole.

Nyota ambao wamethibitisha kutoa burudani katika onyesho hilo ni pamoja na Msaga Sumu, Dulla Makabila, Shilole, Eddu Boy na Pink.

Akizungumza jana jijini, Mratibu wa onyesho hilo, Soud Brown, alisema kuwa shoo hiyo imepelekwa Mazense kwa lengo la kutoa burudani kwa wakazi wa eneo hilo ambalo lina mashabiki wengi wa muziki wa Singeli.

Brown alisema kuwa wanaamini kila msanii waliyemchukua atatoa burudani kwa kiwango cha juu na kuimarisha soko la kazi ya muziki wanaoufanya.

"Lengo kuu la kupeleka onyesho Mazense ni kuwapa burudani karibu, haijawahi kufanyika onyesho lenye muunganiko wa wasanii wa aina hii, naamini itakuwa ni moja ya burudani zitakazowateka mashabiki wa muziki hapa jijini," alisema mratibu huyo.

Aliongeza kuwa wasanii hao watatumbuiza nyimbo zao mpya na zile za awali zilizowatambulisha kwenye tasnia hii ya muziki bila kusahau ulinzi utakuwa wa uhakika wakati wote.

Habari Kubwa