Nandy: Kolabo na Wizkid itapendeza

20Nov 2017
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nandy: Kolabo na Wizkid itapendeza

MSANII wa muziki wa Bongo Fleva na mshindi wa tuzo ya Afrima ya Mwanamuziki Bora wa Kike Afrika Mashariki, Faustina Charles 'Nandy', amesema anafikiri kufanya kolabo na nyota wa Nigeria, Wizkid.

Faustina Charles 'Nandy'.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Nandy alisema tayari amepata mawasiliano na menejimenti ya msanii huyo wa Nigeria na anafikiria kumshirikisha kwenye nyimbo yake kwa siku zijazo.

"Ni jambo ambalo limekuwa kwenye ndoto zangu, nimepata bahati ya kukutana naye Nigeria nilipokwenda kwenye utoaji wa tuzo na tumebadilishana mawasiliano, nataka ndoto yangu itimie kufanya wimbo na Wizkid kwa sababu ni mmoja wa wanamuziki ninaowakubali zaidi," alisema Nandy.

Aidha, msanii huyo amesema anawashukuru Watanzania kwa sapoti yao iliyochangia kushinda tuzo hiyo kubwa.

"Haikuwa kitu rahisi kushinda, nilikuwa na shindana na wasanii wakubwa kama Lady Jay Dee, Victoria Kimani, lakini nashukuru
Mungu nimefanikiwa kushinda tuzo hii," alisema Nandy.

Alisema kwa sasa anajipanga kutoa burudani na kitu kipya kwenye hitimisho la tamasha la Fiesta litakalofanyika mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia kitendo chake cha kuzungumza kiswahili wakati alipokabidhiwa tuzo hiyo kwenye hafla iliyofanyika jijini Lagos, Nandy alisema aliamua kufanya hivyo kutangaza Lugha ya Tanzania.

"Wapo ambao walitumia Kifaransa kushukuru wakati walipokabidhiwa tuzo zao, na mimi niliamua kutumia Kiswahili kwa sababu ni lugha yangu na naitangaza, si kwamba sifahamu Kiingereza hapana, niliamua tu kutumia Kiswahili," alisema.

Habari Kubwa