Nandy sasa balozi taulo za kike Flowless

08Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Nandy sasa balozi taulo za kike Flowless

MWANAMUZUKI wa kizazi kipya, Faustina Mfinanga, maarufu kama Nandy, ametangazwa kuwa balozi wa taulo za kike za Flowless zinazotengenzwa na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya T-Marc.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kuchaguliwa, Nandy alibainisha kwamba kuteuliwa kuwa balozi wa taulo hizo za kike kumetokana mafaniko yake katika muziki ambao umekuwa ukiburudisha jamii, pamoja na imani waliyonayo T-Marc kwake hususan kwenye uwezo wa kuwafikishia ujumbe jamii.

Nandy alisema kuteuliwa huko kuwa balozi wa taulo za kike za Flowless atahakikisha wanawake nchini wanalinda afya zao kwa kuzitumia.

“Ninazijua taulo za kike za Flowless ni kwa ajili ya wanawake wenye ndoto kubwa na wanaojiamini na kuwa tayari kupambana kufikia malengo yao kimaisha siku zote, Ni taulo za kike imara zenye ubora wa hali ya juu na zenye Aloe Vera kukuweka huru muda wote unapokuwa kwenye hedhi, licha ya ubora inauzwa Sh. 3,000 kwa pakiti moja yenye taulo 10,” alisema.

Mkurugenzi wa biashara jamii wa T-Marc, Flavian Ngole, alisema Nandy amekuwa na mchango mkubwa katika jamii hususan katika kuelimisha, kujiamini, kujituma, kuchapa kazi kwa malengo na ushawishi mkubwa alionao kwa vijana wengi wa kike ndani na nje ya nchi.

Alisema lengo la T-Marc ni kuwafikishia ujumbe wanawake wote ndani na nje ya nchi kuhusiana na umuhimu wa kupitia taulo hizo za kike, kwamba imeona ni vema kumtumia Nandy ili awafikishie ujumbe wanawake wote.

Ngole alisema: “Taasisi inatambua nafasi ya sanaa katika jamii, na kwani sanaa inaweza kufanya kazi kubwa kwa jamii na ndiyo maana tutaendelea kuwatumia wasanii wa hapa nchini kuzungumza na Watanzania kuhusiana na bidhaa yetu, kama unavyoona tumemtumia Nandy kutangaza bidhaa hii ya taulo za kike za Flowless”.

Habari Kubwa