TCRA, wasaniii wafikia muafaka

26Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
TCRA, wasaniii wafikia muafaka

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewaagiza wasanii walioingia mikataba na kampuni za simu au mawakala kwa ajili ya kutumia kazi zao kama miito ya simu ambao hawajalipwa stahiki zao, wawasilishe madai yao katika ofisi hizo kwa ajili ya kupatiwa haki zao.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, PICHA MTANDAO

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, aliyaeleza hayo, muda mfupi baada ya kumaliza kikao na wasanii na mawakala waliokuwa wakijadili kuhusu kutokuwapo na mgawanyo sawa wa malipo ya miito ya simu baina ya wasanii wa muziki, kampuni za simu na mawakala wanaotumia kazi za wasanii.

Katika kikao hicho, walikubaliana malipo kuwa kwa kipindi cha miezi sita yakutafuta suluhu ya kudumu, malipo ya kazi za wasanii, mawakala, kampuni za simu na mtoa huduma yawe asilimia 50 kwa 50 kabla ya kuja na mfumo rasmi.

Aliongeza kuwa wamekubaliana kuwapo uwezekano wa msanii kusaini makubaliano ya kazi zake kutumika kama miito ya simu katika kampuni husika ya simu moja kwa moja na endapo atataka kutumia wakala afanye hivyo.

Pia walikubaliana kuwa kampuni za simu ziwasilishe TCRA mgawanyo halisi wa gharama za utayarishaji wa kazi hizo za wasanii ambazo hutumika kama miito ya simu.

Mhandisi Kilaba, alitaja azimio lingine ni TCRA kuangalia uhalisia wa mikataba inayoingiwa baina ya kampuni za simu na mawakala au wasanii kuona kama ni rafiki katika mazingira ya biashara ya miito ya simu.

“Mpaka mwezi wa June mwaka huu, tutakuwa tumeshaangalia namna ya gharama watakazokuwa wanalipana kati ya kampuni za simu, mawakala na wasanii,” alisema Mhandisi Kilaba.

Habari Kubwa