Ufaransa kuleta sanaa ya msosi

18Mar 2019
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ufaransa kuleta sanaa ya msosi

UBALOZI wa Ufaransa hapa nchini umeandaa sanaa ya kutayarisha vyakula vya kiutamaduni wao kama sehemu ya kutunza mazingira.

Hayo yalisemwa  jijini Dar es Salaam na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alifafanua kuwa nchi yake ina lengo la kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na utamaduni.

Alisema tukio hilo litafanyika Machi 21, mwaka huu ambapo watakuwa wanasherehekea na kutambua tamaduni zao kwa Tanzania.

Clavier alisema  nchi hiyo imeongeza pia misaada yake zaidi ya mara mbili iliyotolewa mwaka uliopita na kwamba inapenda kuona Tanzania pia inafikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda mwaka 2025.

Balozi Clavier alisema siku hiyo inayotambulika kama 'Gastronomy Day' kutakuwa na vyakula vya aina mbalimbali ambavyo vitaandaliwa hapa nchini na wapishi wataalamu kutoka Ufaransa, vinywaji kama mvinyo na shampeni pamoja na burudani pia kutoka Ufaransa.

Balozi huyo aliipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kudumisha tamaduni zake hapa nchini na hasa katika upande wa vyakula jambo ambalo ni mfano nzuri.

Alisema anafurahi kuishi Tanzania na angependa atakapostaafu arudi kuwekeza katika sekta hiyo ya utamaduni hususan kwenye vyakula.

Aidha, Clavier alisema nchi yake inaungana na mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira ya baharini unaotokana na matumizi mabaya ya plastiki.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Hoteli ya Hyatt, Garry Friend, alisema kuwa wanatarajia kupokea mpishi mkuu kutoka Ufaransa, Francois Lucchesi ambaye atashirikiana na wapishi wengine wa hoteli hiyo kuandaa chakula hicho.

"Tunashukuru sana kwa heshima ambayo Tanzania na hoteli yetu imepewa na ubalozi wa Ufaransa kuandaa chakula hiki, tunawaalika watu wote kuja kushiriki tukio hili la kihistoria," alisema.

Alisema tukio hilo la kitamaduni litajenga uwezo wa wapishi wa hapa nchini katika kuandaa chakula cha nchini Ufaransa pamoja na kujifunza mambo mengine ya nchi hiyo.

Habari Kubwa