Chadema, CCM vyalaani mabango ya ubaguzi Z'bar

13Jan 2016
Nipashe
Chadema, CCM vyalaani mabango ya ubaguzi Z'bar

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na Chama Cha Mapinduzi (CCM), vimelaani kuhusu dalili za kuibuka kwa ubaguzi wa kisiasa nchini kufuatia ujumbe wa kibaguzi ulioandikwa: 'Machotara Hizbu Zanzibar ni Nchi ya Waafrika,' unalenga kuwagawa Watanzania.

Ujumbe huo ulibebwa katika moja ya mabango na mwananchi mmoja wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja jana.

Katika taarifa za vyama hivyo vyenye upinzani mkubwa wa kisiasa nchini, kwa nyakati tofauti zimeelezea kusikitishwa na ujumbe huo.

Kwa upande wake, Chadema kimesema kwa namna bango lenye ujumbe huo, ni vigumu kuamini kuwa liliibuka ghafla kama vile kitambaa cha mfukoni.

Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jioni na chama hicho kupitia Idara ya Mawasiliano na Habari.

Viongozi wakuu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Kurugenzi za chama, watendaji na wataalam wake, wamejichimbia mkoani Kilimanjaro kwa siku kadhaa sasa wakiendelea na vikao vya tathmini na uchambuzi ambao kwa kawaida hufanyika kila mwanzo wa mwaka, vikiitwa 'retreats'

"Chadema tunalaani na kupinga kwa nguvu zote mabango, mikakati, tabia na chembechembe za ubaguzi wa aina yeyote, ukiwamo huu wa kisiasa ambao sasa unaanza kusakafiwa na kwa sababu hiyo, tunaamini wanaobeba ajenda hii hawataishia hapo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

"Bali watazidi kutugawa Watanzania. Chadema kwa kusimamia misingi yake na kuzingatia kikamilifu misingi ya taifa letu hasa haki, uadilifu, utu, umoja na uzalendo; haiko tayari kuona taifa likihatarisha maisha ya jamii kwa sababu ya kikundi cha maslahi ya watu wachache."

Imeongeza wakati taifa na chama hicho vikimtakia Rais,Dk. John Magufuli, afya njema na nguvu ya kutimiza kwa vitendo kauli yake ya kuwa serikali yake haitawabagua watu kwa misingi ya kisiasa, ni vyema serikali ikachukua hatua kuwawajibisha viongozi waliosimamia na kuachia jambo hilo kutokea huko Zanzibar.

Aidha, Chadema kimemkumbusha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu, kwamba kauli za namna hiyo zisipodhibitiwa ni hatari kwa amani ya nchi na usalama wa raia na mali zao.

CCM kwa upande wake, imesem, imesikitishwa na ujumbe huo wenye maudhui ya ubaguzi.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mawasiliano na Umma CCM, Daniel Chongolo, ilieleza kuwa Chama kinaomba radhi kwa ujumbe huo.

Ilisema CCM inapinga na kukemea kabisa fikra, hisia na mitazamo yoyote yenye maudhui ya kibaguzi kupitia ujumbe huo.

“Ujumbe huo siyo tu kuwa una maudhui ya kibaguzi, bali pia unakwenda kinyume kabisa na falsafa na shabaha ya waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 na unapingana na misingi, itikadi ya CCM inayohimiza umoja na mshikamano wa kitaifa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

KARUME AZOMEWA
Na katika hatua nyingine, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, alizomewa na baadhi ya wananchi wakati akiingia na akiondoka katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja wakati wa maahadhimisho hayo jana.

Tukio hilo lilitokea siku moja tangu Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kukitaka chama hicho kimfukuze uanachama kwa madai amekuwa akishirikiana na wapinzani kuzorotesha malengo ya CCM visiwani Zanzibar.

Kitendo cha kuzomewa kiongozi huyo kilianza kujitokeza wakati viongozi wa kitaifa wakiwasili uwanjani na kutangazwa na mshereheshaji mtangazaji wa zamani wa Sauti ya Tanzania Zanzibar, Suleiman Juma Kimea.

Hata hivyo, baada ya kulitaja jina la Dk. Karume, watu waliokuwa wamekaa katika jukwaa la karibu na viongozi wa kitaifa walianza kupaza sauti zao za zomeazomea...“huyooo…msaliti huyooo… msaliti, hatumtaki. Walisikika wakipiga kelele watu hao wengi wao wakiwa na sare za CCM.
Dk. Karume aliendelea na itifaki ya kuwasalimia viongozi wa kitaifa kabla ya kukaa katika kiti, lakini hali hiyo iliendelea kujitokeza tena wakati Rais huyo mstaafu akiondoka uwanjani baada ya kukamilika wa sherehe hizo.

Wakati hayo yakitokea, Dk. Karume alionekana akinyanyua mikono na kuwapungia kama ishara ya kuwasalimia waliokuwa wakifanya vitendo hivyo.

Mkasa huo ulitokea siku moja baada ya Mwenyekiti wa Umoja UVCCM, Sadif Khamis Juma, kukitaka chama kimvue uanachama Dk. Karume kama walivyofukuzwa wanachama wengine baada ya kwenda kinyume na miko na maadili ya chama hicho.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika maahadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Uwanja wa Maisara juzi, alidai kuwa Karume amekuwa akishirikiana na wapinzani kuimaliza CCM kisiasa Zanzibar.

“Tunakitaka chama chetu kuchukua hatua muhimu kama zile zilizochukuliwa mwaka 1987, kilipowavua uanachama akiwamo aliyekuwa Waziri Kiongozi Seif Sharif Hamad na wenzake sita, akafuatia Mansoor Yussuf Himid, Hassan Nassor Moyo na sasa tunataka afukuzwe mara moja Amani Abeid Karume,” alisema Sadif katika mkutano uliohudhuriwa na Rais wa Zanzibar Dk. Shein.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia mkasa wa Dk. Karume kuzomewa.

"Siwezi kuzungumza chochote, Karume alikuwa bosi wangu nyie kama waandishi ndiyo mnatakiwa kuwauliza waliofanya kitendo hicho wamefanya kwa sababu gani,” alisema Waziri Aboud.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inamheshimu Karume kama Rais mstaafu na kumpa sitahiki zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Habari Kubwa