Chikota ataja kilichopaisha asilimia 95 ya Halmashauri kupata hati ina

28May 2020
Chikota ataja kilichopaisha asilimia 95 ya Halmashauri kupata hati ina

Mbunge wa Nanyamba,Abdallah Chikota (CCM) amesema kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha kuwa kati ya halmashauri 185 ziliokaguliwa, halmashauri 176 imepata hati inayoridhisha sawa na asilimia 95.

Mbunge wa Nanyamba,Abdallah Chikota (CCM).

Hatua hiyo amesema inatokana na nidhamu ya matumizi ya fedha katika mamlaka za serikali za mitaa kuboreka kutokana aa usimamizi mzuri uliopo.

Akichangia taarifa ya kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa (LAAC) kuhusu taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za mamalaka za serikali za mitaa kwa mwaka ulioishia juni 30,2019 amesema hayo ni maboresho makubwa na ni tofauti na kipindi cha nyuma.

“Huko nyuma tulipotoka halmashauri nyingi zilikuwa iznapata hati yenye mashaka lakini kwa sasa ni halmashauri 9 sawa na asilimia 5 tu ndio zimepata hati yenye mashaka,hapa unaona kuna nidhamu ya fedha imejengeka,”alisema Chikota.

Chikota ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati ya LAAC amesema pamoja na maboresho hayo bado kuna maeneo ya kufanyia kazi ikiwemo kwenye taratibu za manunuzi ambapo imeonyesha kuna ukiukwaji.

“Kwenye vitengo vya manunuzi ya serikali za mitaa kumeimarika kwa kiasi kikubwa lakini bado kuna dosari kama CAG alivyoonyesha kuwa amefanya ukaguzi wa kina katika halmashauri 74 na kukuta kuna manunuzi ya Sh bilioni 32.4 yamefanywa bila ya kushindanisha kama sheria ya manunuzi inavyotaka,

“CAG pia amefanya ufuatiliaji wa kina kwenye mamlaka za serikali 47 na kukuta manunuzi yamefanyika bila ya kutumia tender board,na hii imechukua kama Sh bilioni  9.2,hapa afisa masuhuli angeweza kuzuia hoja hizi kwa kutumia tender board ambayo ipo kisheria kwenye mamlaka za serikali za mitaa,”aliongeza Chikota.

Kutokana na hilo ameiomba Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kufuatilia udhaifu kama huo kwa halmashauri husika ambapo taarifa ya CAG ipo wazi na imezitaja halmashauri hizo.

“Tujiulize kwa nini maafisa masuhuli wameamua kufanya hivi maana wanaturudisha nyuma, hoja kama hizi hazikuwa na sababu ya kuwepo kwenye taarifa kama hii,”alisisitiza.

Habari Kubwa