Dalili 10 za 'kujiua' taratibu penzini!

13Jan 2016
Lete Raha
Dalili 10 za 'kujiua' taratibu penzini!

KUSHUHUDIA uhusiano ukianza kuporomoka taratibu kuelekea mwisho wake ni miongoni mwa yaliyo magumu kupokea kirahisi maishani.

Kama ilivyokuwa wakati wa kuanzana, kumaliza pia huambatana na ishara ambazo ukiwa na weledi wa kuzitafakari unabaini kwamba mambo yameshaharibika.
Wengi hufanya 'ubabe' tu kujiaminisha kuwa wangali salama penzini ilhali dalili zinaonyesha wazi kuwa hakuna tena uhusiano zaidi ya kujifanyisha tu maigizo.
Na dalili hizi huanza taratibu kwani hakuna uhusiano wa kimapenzi unaokufa ndani ya siku moja, kimsingi.
Pale unapoona makosa mengi toka kwa mwanaume dhidi yako utambue kuwa hapo ndipo mvuto wake kwako unapozidi kupungua na uhusiano kwa ujumla kuwa mchungu kuelekea kifo.
Hakuna ubishi kwamba hakuna aliyekamilika katika mambo yote na kila mmoja ni mbaya katika eneo fulani lakini unapopenda huwezi kamwe kubaini mapungufu yaliyopo kwa mwenzi wako.
Na kuimarisha uhusiano ni pamoja na kufanya jitihada kubeba mapungufu (yasiyo la lazima) kwani kila mmoja amezaliwa na kukua katika tamaduni zake na tabia pia zisizoweza kamwe kufanana.
Unapoingia katika uhusiano ni lazima utambue kwamba wewe peke yako huwezi kamwe kuujenga pasipo uwezo kamilifu wa mwanaume wako na pindi mambo yatakapoanza kwenda mrama, uwe kwenye nafasi ya kubaini dalili mapema pia.
Kumridhidha mwanaume unayempenda inapaswa kuwa miongoni mwa vipaumbele vyako ili pasiwe na mchango wako wa moja kwa moja katika tatizo (kama unampenda kwa dhati).
Lakini kabla uhusiano haujafa, zipo dalili ambazo unapaswa kuzisoma kama wataalamu wa afya wanavyoshauri dalili mbalimbali za maradhi kama njia bora ya utatuzi wa tatizo husika.

1. MIJADALA HAFIFU
Yanakuwepo maeneo (kitabia, kimatendo n.k) ambayo unatamani mwanaume wako abadilike au ajiboreshe zaidi. Kama utaamua kuyakalia kimya na kupuuza wakati nafsini mwako yanakukera na kukukwaza, ni dalili ya kufa kwa uhusiano taratibu.

2. UWONGO
Uongo hauepukiki sana katika mapenzi. Sawa. Lakini fahamu ya kwamba jinsi unavyozidisha udanganyifu kwake ndivyo uaminifu katika mapenzi unavyopungua siku hadi siku na uaminifu unapopotea katika uhusiano ni tatizo! haupo tena.

3. KUTOCHANGIA
Hakuna anayeunda uhusiano peke yake. Unahitaji wawili na ndio maana ukaitwa hivyo. Uhusiano unahitaji uwiano na mchango sawa wa kila mmoja katika kuujenga.
Pasipokuwapo na uwiano sawa katika kuchangia uhai wa uhusiano wowote hasa wa kimapenzi, tambua ya kwamba nafasi yake kudumu ni ndogo mno.

4. MAHABA YA KUTOSHA
Uhusiano wa kimapenzi usio na mahaba unaboa. Na njia yakufanikisha hili ni kuhakikisha unatambia vionjo vinavyomfurahisha na kumfikisha mwenzi wako na kwenda navyo sambamba. Muhimu ni kila wakati kusisitiza mvuto baina yenu.

5. LAWAMA
Ndio! Endelea kumlaumu tu mwanaume wako kwa kila jambo liendalo kombo katika uhusiano wenu na uushuhudie ukifa kifo cha kawaida. Kila dosari unakwenda kumtwisha lawama tu zisizokwisha na elewa kwamba kadiri unavyolaumu ndivyo unavyozidisha kero katika uhusiano na kuufanya upoteze thamani ya kuwepo.

6. MAWASILIANO
Sio kwa kupigiana simu tu au kutumiana ujumbe mfupi kila wakati bali mawasiliano katika kushirikisha kila mmoja katika ratiba ni muhimu.
Weka wazi ratiba zako, kazi zako au masuala yako ya familia na marafiki kwa mwanaume wako kwani kumuacha gizani asijue yako vya kutosha, hukuweka mbali naye na kuhatarisha uhusiano husika.

7. UBUNIFU
Kubuni mapya na kujibadilisha ni jambo muhimu mapenzini. Ukiwa 'wa kawaida' sana kila wakati inamchosha mwanaume na kupoteza thamani yako na ya uhusiano wenu kwa ujumla.

8. UPOLE WA PLASTIKI
Unajifanya kuwa mpole katika kila jambo ili kumvutia akuone mkimya.! Utafanya hivi mpaka lini? Miongoni mwa sumu kubwa katika mahusiano ni kufanya maigizo. Katika uhusiano wa dhati wa kimapenzi, kila mmoja anahitajika kuwa 'yeye'!

9. MUDA MBOVU
Panapokosekana muda wa pamoja na mwanaume wako kutokana na sababu mbalimbali kama 'ubize' kupitiliza fahamu ya kwamba unapalilia kifo cha penzi lako.
Kutumia muda pamoja naye huimarisha bondi ya uhusiano na kumaanisha mengi mazuri yasiyotosha katika ukurasa mmoja.

10. MATARAJIO MAKUBWA
Unamtaka ajue unachohitaji kwake bila kumwambia? Unamtaka akumbuke kila kitu licha ya kuwa na mambo mengi yanayohitaji umakini wake?
Sawa, mpo katika mapenzi na uwepo wa kila mmoja nafsini kwa mwenzake una maana lakini ni binadamu wa kawaida wa kufanya mengine pia. Tarajia mengi uvune mabaya na tarajia machache uone jinsi mwanaume wako atakavyojali.

Habari Kubwa