DK JOYCE BAZIRA Kutoka mtafuta habari hadi gwiji wa taaluma

26Jan 2016
Jackson Kalindimya
Nipashe
DK JOYCE BAZIRA Kutoka mtafuta habari hadi gwiji wa taaluma

Mwaka 1994 Joyce Bazira aliajiriwa na kampuni ya The Guardian akiwa mwandishi wa kawaida.Katika safari yake hiyo ya taaluma, baada ya miaka kadhaa alijikuta akikwea na kushika nafasi nyeti katika gazeti, kuwa Mhariri wa Habari wa gazeti la Alasiri lililokuwa linachapishwa na kampuni hiyo na baadaye alipandishwa kuwa Mhariri wake.Mwaka 2009, aliacha kazi ili kwenda kutimiza ndoto yake ya kielimu, katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino,Mwanza ambako alivuka milima na mabonde hadi siku 10 zilizopita akiwa kati ya wahitimu wawili wa kwanza,akiambatana mwanamke mwenziwe mwanahabari Kanaeli Kaale, kuwa wa kwanza katika historia ya nusu karne ya Chuo kutunikiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma

Swali:Dk Joyce Bazira ,wewe ni miongoni mwa wanawake wawili kupata Shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano ya Umma(PhD), kwa mara ya kwanza kabisa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kilichoanzishwa miaka 50 iliyopita,unajisikiaje?
JIBU:Najisikia furaha kupata mafanikio hayo makubwa, nikiwa miongoni mwa wanawake wa kiafrika ambao mazingira ya upatikanaji wa elimu sio rahisi.
Najisikia ni mtu ninayewiwa sana kurudisha matunda yangu kwa watu wangu,hasa wanaoniangalia kama ni mfano kwao (role model) kutekeleza matarajio yao ni changamoto kubwa kwangu.
Swali: Dk Joyce wewe ni mama, mke wa mtu mwenye dhamana kubwa kwa jamii,uliwezaje kuugawa muda wako sasa umefanikiwa kufikia ngazi hiyo?
JIBU: Changamoto kubwa sana ni namna ya kuugawa muda. Nililitambua hilo kwa kuamua kujinyima kufanya mambo yangu binafsi (social life) na mambo ya kijamii kuyafanya kwa uangalifu sana ili yasiathiri maendeleo yangu kama vile misiba, shule kwa watoto na mengineyo.
Nakumbuka wakati Prof.Robert White anazindua kozi yetu alitusomea (amri) masharti 10 ya kuzingatia unaposoma kozi ya uzamivu (PhD) ambayo yalitusaidia sana kutupa picha ya majukumu tunayotarajia kukabiliana nayo.
Miongoni mwa masharti hayo ni kusoma vitabu zaidi ya 1000. Pili, kuhakikisha kuwa program unaipa muda wako wote.Yaani kama unataka kufanikiwa inabidi kuipa kisogo dunia nyingine. Hivyo ndivyo nilivyofanya.
SWALI:Nini siri ya mafanikio yako?
JIBU: Nimekuwa na malengo ya kujiendeleza na kutafuta elimu kwa bidii tangu mwaka 1994, nilipoajiriwa katika Kampuni ya The Guardian kufanya kazi chumba cha habari nikiwa mwandishi wa habari wa kawaida. Nilikuwa najua ninachokitaka na kwamba kitu hicho hakiji hivihivi tu lazima ukipiganie au ukitafute kwa juhudi na maarifa.
Pili, kupenda kufanya kile ninachopenda kukifanya.Mimi napenda kusoma.Tangu nikiwa chumba cha habari nilikuwa natafuta fursa zote kwa ajili ya kujijengea uwezo na kuzifanyia kazi kikamilifu bila ya kulazimishwa.
Tatu, ni kuungwa mkono na familia yangu.Kutafuta elimu kwa namna yoyote ile yahitajika uwe na raslimali. Mume wangu Chifu Fred Ntobi alinielewa na kuniunga mkono sana. Ametumia raslimali nyingi kunilipia ada, kuninunulia vitabu na kugharamia safari zangu kwa ajili ya kutafuta elimu.Yeye ndiye mfadhili wangu.
Alikuwa akinununulia vitabu ambavyo nikipita kwenye maduka ya vitabu na kuona bei zake nilishtuka sana.Ukweli amejitoa sana kwa ajili yangu ,hata nilipojaribu kumuuliza kwa nini unafanya yote haya, alisema anafanya hivyo kwa sababu anaamini akili yangu ni nzuri na kuahidi kutumia kile alichonacho kuhakikisha natimiza ndoto zangu.
SWALI: Dk Bazira ulikuwa unafanya kazi, Mhariri wa gazeti la Alasiri ukilipwa mshahara uliokuwezesha kukabli mahitaji ya msingi na pengine ziada kwa ajili ya maendeleo yako.Nini kilikufanya ukaacha kazi ?
JIBU:Niliacha kazi mwaka 2009 wakati huo nikilipwa mshahara mkubwa tu.Nililazimika kufanya hivyo kwa sababu, safari ya elimu niliyoianza ilikuwa inahitaji kutumia muda wangu wote. Siku zote mshika mawili moja humponyoka.
Nisingeweza kufanya kazi za chumba cha habari, kisha nisome vitabu vingi kwa ajili ya kujenga hoja za kitaaluma isingekuwa rahisi .
Ndio fedha ni nzuri ,lakini kutekeleza mafanikio ya kitaaluma ilikuwa ndoto yangu niliyopania kuhakikisha inatimia.Fedha niliamini kabisa kuwa zitakuja tu.
Niliamua kutoa sadaka kazi na mambo yangu mengine mazuri na pengine muhimu kwa ajili hiyo.Ilibidi mambo hayo kuyaahirisha yasubiri wakati wake mwingine .
Ajabu ya Mungu, baada ya kuanza masomo hayo mwaka wa kwanza tu nikaanza kupata kazi za kitaaluma za kufanya katika muda wangu wa ziada ikiwemo kupitia taarifa mbalimbali na kutumiwa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari na mihadhara ya kitaaluma katika Shule ya Mawasiliano ya Umma na Uandishi wa Habari (IJMC) ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Fedha ikaanza kunifuata na kunifanya nisijute kuchukua maamuzi hayo. Kazi zilinifuata hadi nikawa nazikataa.
SWALI:Changamoto gani ulizokabiliana nazo na ulizikabili vipi?
JIBU:Changamoto kubwa ni kuugawa muda wangu kwa mambo yote muhimu na kutoa sadaka yale mengineyo licha ya kuwa ni muhimu, lakini unalazimika kuyaacha kama vile hayakuhusu.
Miongoni mwa mambo hayo ni kusoma vitabu vya hadithi (novels), kuangalia sinema na kusafiri hapa na pale.Nilikuwa nayapenda sana mambo hayo lakini nikalazimika kuyaacha. Mwaka wa kwanza sikusafiri kabisa.
Pili ni kuhakikisha kuwa unaishi maisha ya kitaaluma.Yaani kuhakikisha kuwa, kile unachokisema kinakuwa na nguvu ya kitaaluma, yaani kinaungwa mkono na andiko au ushahidi wa kitafiti. Lengo ni kuhakikisha kuwa, siiangushi taaluma ninayosomea pamoja na hadhi ya chuo changu.
Tatu, utafiti wangu niliufanya ulihusu Uandishi wa Habari kuhusu Migogoro na Amani. Niliufanyia katika kisiwa cha Zanzibar na Kenya. Kwa kuwa nilifanya nje ya nchi ilihitajika gharama kubwa kusafiri na nyinginezo kwa muda wote huo.
SWALI: Kwa nini uliamua kufanya utafiti katika eneo hilo?
JIBU: Ni eneo jipya kabisa, ambalo waandishi wengi wa habari hawana uelewa nalo na tumekuwa tukilalamikiwa kuwa hatufanyi vizuri na wakati mwingine kuchangia chokochoko na isitoshe kuna machapisho machache katika eneo hilo. Changamoto hiyo, ilinifanya nishawishike kulifanyia utafiti na kujionea kilichomo humo ili kusaidia kuleta ufumbuzi wa migogoro inayotokea na kusababisha hasara kwa mataifa makubwa na madogo. Lengo ni kuona kama tunaweza kusaidia kuleta amani.
Jambo jingine ni kwamba kuwa na shauku ya kulishughulikia eneo hilo. Kuna waandishi wazuri, lakini hawajaingia katika eneo hilo ili kuweza kusaidia kuchangia kuleta amani hivyo kujikuta wanafanya yale ambayo hayakupaswa kufanywa ili kudumisha amani na kuepusha migogoro.
SWALI:Wewe ni mwandishi wa habari unatambua majukumu na muda wao wanavyokimbizana.Je ,suala la waandishi wa habari kujiendeleza hasa wanawake lina nafasi yoyote kwa maendeleo yao na taaluma kwa ujumla?
JIBU:Suala la elimu halikwepeki.Mwandishi lazima ujiendeleze kama unataka kuandika kwa usahihi na kufanya uchambuzi makini katika hadhira ya sasa inayoshiriki kupata habari na taarifa katika vyanzo vingine (social media) kulingana na maendeleo ya teknolojia.
Uchambuzi makini na uelewa mpana ndio utakaomfanya mwandishi aihudumie jamii yake vyema. Tusiwape yale tunayotaka, tuwape yale ambayo ni ukweli unaojitosheleza ili kuwawezesha wafanye uchambuzi wao kulingana na mahitaji yao.
Waandishi wawe na kiu ya kupata elimu na hilo kwa namna yoyote ile linawezekana na muda sio tatizo hata kidogo wakiwemo wanawake. Wasiangalie kipato chao au majukumu yao. Mimi nimejaribu nimeweza toka chini kabisa kwa nini wao washindwe? Kikubwa kinachotakiwa ni kuwa na dhamira ya kusoma na maamuzi kisha kujitahidi kutimiza dhamira hiyo.
Ulimwengu wa sasa kuna nafasi kubwa kuongozwa na wanawake katika ngazi za maamuzi. Hapa nchini sasa hata nafasi za juu kabisa zinashikwa na wanawake. Msukumo huo upo hata katika vyumba vya habari lakini watashindwa kushika nafasi hizo kama hawajajitosheleza kulingana na matakwa ya kielimu hata kama wanastahili ni vigumu kutekelezewa ili kushika dhamana hizo.
SWALI:Zama hizi kulingana na maendeleo ya teknolojia kuna upatikanaji wa habari kupitia mfumo mpya (social media) ambao yawezekana ni wa kasi zaidi ikilinganishwa na mfumo wa asili wa vyombo vya habari uliozoeleka. Waandishi wa habari na vyombo vya habari vifanye nini ili kuendana vyema na mabadiliko hayo?
JIBU:Hatuwezi kuzuia mabadiliko hayo.Tuchukue hiyo kuwa ni changamoto ya kuifanyia kazi. Habari zinazopatikana huko tuzichukue kwa umakini na kuzifanyia kazi kwa kina na usahihi ili kuifahamisha hadhira yetu inayotutegemea na kutuamini linapokuja suala la upashaji habari.
Vyombo vya habari vinaaminika na umma kama vitajenga mazingira ya kuaminika.Tuandike vizuri,kwa usahihi,kwa kina na kwa kirefu tusiige yanayofanyika kwenye social media kutoa habari ambazo hazijafanyiwa kazi.
Waandishi wanatakiwa kuhakikisha kuwa hawapotezi kuaminika kwao kwa jamii ili waendelee kufanya vizuri.Ni rahisi sana kupoteza kuaminika kama hufanyi mambo kwa usahihi yanayoaminika na jamii na kujitahidi kupata habari mpya kila wakati, yaani kuwa kiongozi.
Ukipoteza kuaminika na umma ni kazi kubwa sana kurudisha imani hiyo.Utawadanganya watu siku ya kwanza, lakini wakishagundua kuwa husemi ukweli hutawadanganya milele watakuepuka. Jamii ya sasa ina vyanzo vingi vya kupata habari.Tusiruhusu kujifikisha huko.
Lazima uwajibike kwa nafsi yako kama binadamu,taaluma yako ,chombo cha habari unachokifanyia kazi (mwajiri wako) na umma unaohudumia.
SWALI: Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ni miongoni mwa zile ambazo Tume ya Jaji Nyalali iliziorodhesha kuwa hazifai na zinatakiwa kufanyiwa marekebisho. Sheria hiyo bado ipo na inafanyiwa kazi unaizungumziaje?
JIBU:Wakati umefika sasa tupate sheria ambayo itawafanya waabndishi wafanye kazi katika mazingira rafiki na wananchi wapate habari kwa uhuru kulingana na sheria hizo.Wakati wa kutumia sheria kama rungu umepitwa na wakati.
Wito wangu kwa waandishi wa habari, tuwajibike kikamilifu tusisubiri kushushiwa rungu kwa sheria hizo.Watanzania ni waelewa sana.
Kazi tunayoifanya ina heshima kubwa sana hivyo baadhi ya watu wakipata nafasi wanaweza kutuwekea vikwazo hasa wenye mambo yao ambao sio wasafi.Tuwajibike kwa jamii.Hii sio kazi ya utani.Ina dhamana kwa jamii.
Ninachoshauri linapokuja suala lenye maslahi mapana ya kijamii ni vyema vyombo vyote vya habari kusimama kwa pamoja kuushughulikia uovu hadi waovu wakose usingizi.
Tuache tofauti zetu kwa kila chombo kufanya peke yake tunapokuwa na ajenda zinazogusa maslahi mapana tuwe na sauti ya pamoja.
SWALI:Ni mambo gani katika safari yako ya maisha yalikufurahisha au kukusikitisha katika maisha unayoyakumbuka sana?
JIBU:Nilipompoteza mtoto wangu Daniel, ni tukio ambalo ni vigumu kulisahau. Amefariki akiwa bado mdogo sana akiitafuta elimu. Nimesoma na matokeo haya nayatunuku kwake.
Tukio jingine ni la Mama mkwe wangu alifariki mwaka 2013. Alikuwa ananiunga mkono sana alipofariki nilipungukiwa sana.Na mwaka 2014,nilifiwa na Baba mkwe wangu nikiwa katika kipindi kigumu cha masomo yangu, mungu awarehemu.
Kwa upande wa furaha ni pale nilipotangazwa kupata tuzo ya shujaa wa Bima ya Afya nikiwa miongoni mwa waandishi saba mwaka 2013 kwa kazi ya uandishi niliyoifanya miaka mingi
Mwaka jana niliteuliwa kuwa katibu wa majaji wa shindano la kuwapata waandishi bora (EJAT) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na kuaminiwa kufanya kazi nyingine za kitaaluma.
SWALI:Msomi wa daraja lako, jamii itarajie nini kutoka kwako?
JIBU:Nipo tayari kushirikiana ujuzi wangu na jamii. Jamii ikiona namna gani inaweza kunitumia nipo tayari kuwatumikia kwa uwezo na akili yangu yote kurudisha shukrani kwao
SWALI: Kila ukiangalia safari yako ya maisha na elimu kwa ujumla ni nani hasa unamkumbuka na kumshukuru sana
JIBU:Watu wengi wamechangia mafanikio yangu katika ngazi tofauti kuanzia familia yangu, wazazi, ndugu, jamii na mume wangu Chifu Frederick Ntobi wa Masanza, Magu, Mwanza ambaye amejitoa sana kwangu kwa hali na mali
Baadhi ya marafiki walioniunga mkono kwenye safari yangu ya kitaaluma ni pamoja na Peter Ouma, Kiondo Mshana na Alakok Mayombo.Wote kipekee kabisa nawashukuru sana.
SWALI: Je, una maoni gani mengine unayopenda kuyazungumza ambayo sikuyagusia katika mahojiano haya?
JIBU:Naipongeza sana Kampuni ya The Guardian niliyojiunga nayo mwaka 1994 wakati huo nikiwa na umri mdogo wa miaka 22.Imenijengea mazingira ya kukua kitaaluma wakanipa fursa za kusafiri kuitembelea dunia huku nikizidi kuimarika.Nikapewa dhamana ya kupanda daraja hadi kuwa Mhariri wa gazeti la Alasiri.Niliwaaga nikaondoka kwa sababu majukumu ya kusoma wakati huo hayakunipa fursa tena.Nawashukuru sana kwa yote waliyoyafanya kwangu .
Nawashauri kuwa, wakigundua kuwa kuna wafanyakazi wenye vipaji vya kusoma au kufanya mambo ambayo yatakuwa na manufaa kwa jamii wafanye hivyo.
Pia vyombo vingine vya habari vijenge mazingira ya kuwafanya wafanyakazi wao wakue kitaaluma wanapoona wana vipaji hivyo.

Habari Kubwa