Dk. Mengi ahimiza upendo, mshikamano katika jamii

25Jan 2016
Salome Kitomari
Nipashe
Dk. Mengi ahimiza upendo, mshikamano katika jamii
  • "Sala, imani, kuliombea taifa, upendo na mshikamano ni mambo muhimu katika jamii, vinginevyo wenye ulemavu watapata matatizo makubwa kama ya unyanyapaa."

MWENYEKITI Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amesema upendo na mshikamano katika jamii ndiyo vitakavyosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, akigawa chakula kwa mmoja wa walemavu wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichokiandaa kwa ajili ya watu wenye ulemavu, jijini Dar es Salaam jana.

Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichokiandaa kwa ajili ya watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mengi alisema kuna Watanzania wengi wenye uwezo ambao wakiamua wanaweza kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na kuwafanya wafurahie maisha.
"Popote palipo na upendo ni salama kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa watawashika mkono, mwenye upendo hatamnyima chakula mwenye ulemavu, atahakikisha anapata mahitaji ya lazima, hakutakuwa na unyanyapaa, palipo na upendo na mshikamano wa kitaifa wenye ulemavu hawawezi kupata matatizo yoyote," alisema na kuongeza:
"Sala, imani, kuliombea taifa, upendo na mshikamano ni mambo muhimu katika jamii, vinginevyo wenye ulemavu watapata matatizo makubwa kama ya unyanyapaa."

Aidha, Dk. Mengi aliwataka wenye ulemavu kukataa kuitwa wenye ulemavu, kwani kuwa wenye ulemavu hakuwaondolei utu na ubinadamu wao.
"Msikubali kuitwa walemavu, mkikubali kuitwa hivyo ni kuongeza unyanyapaa wa utu na ubinadamu wenu. Ni wajibu wenu kuelimisha, kufundisha na kuijulisha jamii ili wawaone nyie ni wanadamu wenzao na wote ni maua ya Mwenyenzi Mungu," alisema.
Alisema miaka yote amekuwa akizungumzia changamoto zinazowakabili wenye ulemavu na kwamba nchi ina uwezo wa kuwahudumia kwani Watanzania wasio na ulemavu wana nafasi ya kuwasaidia kuondokana na matatizo yanayowakabili.
AMPONGEZA JPM

Dk. Mengi alimpongeza Rais Dk. John Magufuli, kwa kuwateuwa watu wenye ulemavu kushika nafasi muhimu katika serikali yake, akisema ni jambo linaloonyesha ana imani na wenye ulemavu kwamba wana uwezo wa kufanyakazi sawa na watu wasio na ulemavu.
"Matumaini na sala zetu ni Rais kuendelea kuwapa madaraka watu wenye ulemavu katika serikali na mashirika ya umma pale ambako wana uwezo wa kielimu na kufanyakazi mbalimbali," aliema.
SHIVYAWATA YAELEZA CHANGAMOTO

Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata), Ummy Nderiananga, alimshukuru Dk. Mengi kwa kulijali kundi hilo kwa kukaa na kula nao chakula jambo ambalo ni ishara ya upendo kwao.
Aidha, alieleza changamoto zinazokabili kundi hilo kuwa ni kukosa miradi ya kudumu ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi hivyo kubaki kuwa ombaomba na kutoa wito kwa Watanzania wenye uwezo kulisaidia kundi hilo.
Alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu na kwamba watoto wengi wa kundi hilo wanakosa elimu kwa sababu ya kukosa uwezo wa kutimiza mahitaji ya msingi.

Alitaja nyingine ni kukosa ajira licha ya wengi kuwa na vipaji, kukosa mitaji ya kuanzisha shughuli za kujikwamua kiuchumi, mtazamo hasi wa jamii kiasi cha kunyanyapaliwa na kukosa vifaa muhimu kama kuti mwendo, fimbo maalum na vya kusomea.
WALEMAVU WANENA
Mwakilishi wa watu wenye ulemavu kutoka mkoa wa Dodoma, Herzron Lusanyu, alimpongeza Dk. Mengi kwa moyo wa kuwajali wenye ulemavu na kumuomba kuangalia uwezekano wa kuwawezesha kiuchumi ili waweze kujikwamua kutoka katika umaskini.

Habari Kubwa