Dunia yashtushwa na kifo cha Bryant, Obama, Trump wamlilia

27Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Dunia yashtushwa na kifo cha Bryant, Obama, Trump wamlilia

Bingwa mara tano wa ligi ya kikapu nchini Marekani (NBA), Kobe Bryant (41) amefariki katika ajali ya ndege binafsi aina ya Helikopta aliyokuwemo yeye na mtoto wake wa kike Gianna (13) na watu wengine saba kwa mujibu wa ripoti mbalimbali nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali nchini humo zinasema kuwa ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Jumatatu, Januari 27, 2020 kwa saa za Afrika Mashariki wakati nchini Marekani ni majira ya mchana katika eneo la Calabasas, jimbo la California, ambapo helikopta hiyo ilianguka na kuungua huku kukiwa hakuna mtu aliyenusurika.

Baada ya taarifa hiyo, Dunia nzima imeshtushwa na kifo cha gwiji huyo wa mchezo wa kikapu, miongoni mwao ni Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama ambaye aliandika katika mtandao wa Twitter akisema, "Kobe alikuwa ni mtaalamu katika 'court' na alianza katika kitu kingine cha pili. Kumpoteza Gianna ni maumivu makali sisi kama wazazi. Mimi na Michelle tunatuma salamu za rambi rambi na tunawaombea Vanessa na familia nzima ya Bryant kwenye siku hii ambayo haifikiriki".

Naye rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump amezungumzia msiba huo mzito akisema kuwa Bryant licha ya kuwa mchezaji bora wa muda wote wa kikapu, alikuwa ndiyo anaanza katika maisha, aliipenda familia yake na kitendo cha kumpoteza mtoto wake Gianna ndiyo maumivu makali zaidi.

Mkuu wa polisi jijini Los Angeles Alex Villanueva hata hivyo alikataa kutoa utambulisho wa watu hao wengine hadi uchunguzi wa miili utakapokamilika.

 

Habari Kubwa