EFD za bure kuigharimu TRA bn100/-

23Jan 2016
Romana Mallya
Nipashe
EFD za bure kuigharimu TRA bn100/-

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), inasaka zaidi ya Sh. bilioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa mashine za Kieletroniki za kodi (EFDs) 200,000, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli alilowataka wazitoe bure kwa wafanyabiashara.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo

Rais Magufuli alipokutana na wafanyabiashara wa Taasisi ya sekta Binafsi nchini (TPSF) mwishoni mwa mwaka jana, alipendekeza TRA itoe bure mashine hizo ili mamlaka iangalie mapato kutoka kwao. Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, akizungumza na Nipashe jana ofisi kwake alisema wanaendelea kufanya utaratibu wa kupata fedha hizo.

“Wanaohitajika kupewa mashine ni 200,000 ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili… wafanyabiashara watakaopata ni wale wasiosajiliwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ” alisema.

Alisema mara baada yakupata fedha hizo watapanga utaratibu wa jinsi ya kuzigawa na kuzihudumia.

Aliongeza kuwa, wale ambao walinunua mashine hizo kwenye awamu ya kwanza, tayari wamerejeshewa malipo ya gharama za mashine hizo walipopeleka marejesho ya kodi.

Habari Kubwa